Siasa

Wimbi la kuhama vyama lashika kasi kuelekea 2027

Na KEVIN CHERUIYOT November 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa kisiasa wameanza kuhama vyama kwa wingi huku uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027 ukikaribia, kila mmoja akitafuta tiketi ya chama anachoamini kitampa nafasi nzuri ya kushinda.

Katika siku za hivi majuzi, makao makuu ya vyama mbalimbali yamekuwa na shughuli nyingi, huku viongozi na wanasiasa wanaotaka kuwania nyadhifa tofauti wakipokelewa kutoka vyama pinzani.

ODM ni miongoni mwa vyama vinavyopokea wageni wengi, kikilenga kuimarisha ushawishi wake kote nchini licha ya kuwa kitashiriki uchaguzi wa kwanza bila mwanzilishi wake, marehemu Raila Odinga.

Naibu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Kisii Simba Arati amesema chama hicho hakitaisha kufuatia kifo cha Raila, kama baadhi ya wapinzani wake wanavyodai.

Arati alisema ODM bado kina nguvu na milango yake iko wazi kwa wanasiasa wanaotaka kujiunga nacho.

“ODM kiko imara sana na tunawaambia wasubiri waone. Tuko tayari kupokea wanachama zaidi. Wiki ijayo tutapokea wabunge saba ambao wameonyesha nia ya kujiunga nasi kutoka vyama vingine,” alisema.

Miongoni mwa viongozi waliojiunga na ODM ni aliyekuwa Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, aliyeondoka Kanu ya Gideon Moi akiwa ameandamana na madiwani saba walio mamlakani pamoja na wagombeaji wengine.

Poghisio alisema analenga kuwania ugavana wa Pokot Magharibi kwa tiketi ya ODM katika uchaguzi ujao. Alisema chama hicho kina historia nzuri katika eneo hilo na kina nafasi ya kushinda viti vingi vya kisiasa.

“ODM imekuwa chama chenye nguvu Pokot Magharibi. Si mara yangu ya kwanza kuvaa rangi ya chungwa. Nilikuwa mmoja wenu miaka iliyopita kabla ya ODM kugawanyika na nilikuwa mwenyekiti wa kitaifa wa ODM-Kenya. Sasa tunataka kuwezesha ODM kupata ugavana, madiwani 20 na wabunge wanne,” alisema.

Hata hivyo, Poghisio alisisitiza kuwa eneo hilo litaunga mkono azma ya Rais William Ruto kutetea kiti chake mwaka 2027.

Kuhamia kwa Poghisio na wenzake ODM kulifuatia kupokelewa kwa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, aliyehama UDA ya Rais Ruto.

Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda, aliyechaguliwa kwa tiketi ya Kanu, pia ameonyesha nia ya kujiunga na ODM.

Silas Jakakimba naye alipokelewa rasmi ODM baada ya kuondoka UDA. Anatarajia kuwania ubunge Suba Kaskazini mwaka 2027, kiti kinachoshikiliwa na Millie Odhiambo.

Huku ODM ikipokea wanachama wapya, chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) kinachoongozwa na Mbunge wa Gem David Ochieng pia kimekuwa kikivutia wanasiasa.

Mnamo Jumanne kilipokea wabunge Oku Kaunya wa Teso Kaskazini na Joseph Oyula wa Butula, ambao walichaguliwa kupitia ODM.

Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pia kinatarajiwa kupokea wagombeaji kutoka vyama vingine.

Gachagua amedai kuwa wabunge kadhaa waliochaguliwa kwa tiketi ya UDA wanasubiri muda mwafaka wa kuhamia upande wake.

Katika kaunti ya Nairobi, wabunge wote watatu wa Jubilee waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita wametangaza kuwa watatetea viti vyao kupitia DCP.

Hao ni Yusuf Hassan wa Kamukunji, Mark Mwenje wa Embakasi ya Kati na Amos Mwago wa Starehe.

Mbunge wa Kariobangi Kaskazini James Gakuya, aliyechaguliwa kupitia UDA, pia ameonyesha nia ya kutafuta tiketi ya DCP kuwania ugavana wa Nairobi.

Wakati huohuo, vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna linatarajiwa kuvutia wagombeaji wapya.

Winnie Odinga, binti wa Raila na mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ameashiria uwezekano wa kuwania useneta Nairobi mwaka 2027 kupitia ODM au Linda Mwananchi.

Hata hivyo, bado hajafanya uamuzi kuhusu chama atakachotumia, huku akiwaomba wafuasi wake na wanaomfuatilia mitandaoni kumsaidia kuchagua chama kinachofaa.

Mabadiliko haya yanaashiria kuwa safari ya kuwania tiketi za vyama imeanza mapema, huku wanasiasa wakipima nguvu za vyama na nafasi zao za kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027.