• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
4 wanaswa na DCI kwa kuua mshukiwa wa wizi wa kuku

4 wanaswa na DCI kwa kuua mshukiwa wa wizi wa kuku

Na PETER MBURU

POLISI kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) Jumapili waliwakamata wanaume wanne eneo la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega, ambao wanatuhumiwa kumuua mwanamume kwa kumkatakata, kwa madai kuwa alikuwa ameiba kuku.

Maafisa hao kutoka makao makuu ya DCI Nairobi, waliwakamata wanne hao baada ya kanda ya video iliyoonyesha mmoja wa washukiwa, Francis Muse Liseche almaarufu Moi ama Rais, akimkatakata mwanamume huyo, ikienezwa mitandaoni.

DCI kupitia akaunti yake ya Twitter, Jumapili ilisema mwathiriwa alifariki kutokana na kukatwakatwa huko.

“Francis Muse Liseche, almaarufu Moi na Rais aliyerekodiwa katika video akimkatakata mwanamume kwa madai ya kuiba kuku amekamatwa na maafisa wa uchunguzi kutoka Makao Makuu,” DCI ikasema jana.

Idara hiyo ilisema wengine waliokamatwa ni pamoja na mwenye kuku aliyesababisha kuuawa kwa mwanamume huyo.

“Mwathiriwa alikufa kutokana na kukatwakatwa kinyama. Wanne hao; wengine wakiwa Evans Lichoti Ashihundu, 34, Agapitus Ingosi Ang’uswa ,43 na Reuben Smith Shitambasi, 48 watafikishwa kortini Jumatatu (Leo) kukabiliwa na mashtaka ya mauaji,” DCI ikasema.

Idara hiyo ilitahadharisha umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi, ikisema uchunguzi dhidi ya kisa hicho cha mauaji bado unaendelezwa.

You can share this post!

Samboja na madiwani wake watakiwa kutafuta suluhu

Viongozi wa Magharibi wamlilia Rais awape waziri serikalini

adminleo