Mwanahabari abubujikwa na machozi baada ya kuponea kusukumwa ndani
Na RICJARD MUNGUTI
MWANAHABARI alidodokwa na machozi Jumatano kortini baada ya polisi kunyimwa fursa ya kumzuilia siku saba kuhusiana na shambulizi la mfanyabiashara katika hoteli moja jijini Nairobi.
Bw Sangira Stephen Ochola, ambaye picha yake ilisambazwa mitandaoni kutokana na shambulizi la Bw Timothy Muriuki mnamo Aprili 30, 2018 alishindwa kujimudu na kujipata akitiririkwa n amachozi baada ya hakimu mkazi Bi Miriam Mugure kusema “hakuna ushahidi wowote uliomhusisha mwanahabari huyu na kisa cha kutwangwa kwa mlalamishi.”
Mahakama iliambiwa hakuna utambuzi mwingine unahitajika kwa vile picha ya Ochola imeonekana kote ulimwenguni baada ya kuchapishwa na magazeti ya Taifa Leo na Daily Nation.
Mawakili Cliff Ombeta, Nelson Havi , Michael Osundwa , Rodger Sagana na Harun Ndubi walimweleza hakimu polisi wanataka kumtesa mshukiwa.
Akimhoji afisa anayechunguza kesi hiyo Koplo Francis Mwita , Bw Ombeta alimtaka aeleze ikiwa Bw Ochola alitiwa nguvuni wakati mmoja na Mbunge wa zamani wa Kamkunji Simon Mbugua na mabroka Antony Otieno Ombok almaarufu Jamal na Benjamin Odhiambo Onyango almaarufu Odhis mnamo Mei 8, 2018.
Koplo Mwita alikiri aliwatia nguvuni wote wanne wakati mmoja.
“Mbona hukumfungulia mshtaka ya wizi wa mabavu wakati mmoja na Mabw Mbugua, Ombok na Onyango?” Bw Ombeta akauliza.
“Sikuwa nimekamilisha uchunguzi kwa vile kuna washukiwa wengine wanaoendelea kuswakwa na polisi,” alijbu Koplo Mwita.
Koplo Mwita aliomba korti iamuru mshukiwa huyo azuiliwe kwa siku saba ndipo “walalamishi wajitokeze kumtambua kwa vile anashukiwa amehusika katika visa vingine vingi vya kuwashambulia watu.”
Mahakama iliambiwa Koplo Mwita anamtesa mshukiwa huyo.
“Kubali tu unamtesa mshukiwa huyu,” Bw Ombeta alimwambia polisi huyo.
“Hapana,” alijibu Koplo Mwita.
Mawakili Ndubi , Sagana na Havi walisema kile mahakama inaweza kufanya ni kumwachilia mshtakiwa kwa dhamana kwa vile “tayari afisa mkuu wa polisi Ireri Kamande ameshasema hawatamshtaki Bw Ochola.”
Bi Mugure alitupilia mbali ombi la kumtaka Bw Ochola azuiliwe kwa siku saba.
Pia alisema Koplo Mwita hakuwa ameitia saini ombi alilowasilisha kortini akiunga mkono kuzuiliwa kwa mshukiwa huyo.
Korti ilimwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu kisha ikamwamuru afike mbele ya koplo Mwita kuhojiwa.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Mei 14, 2018.