Kimataifa

Biden hatimaye ajiondoa mbio za urais kufuatia shinikizo kwamba uzee umemlemea

Na FRIDAH OKACHI July 21st, 2024 1 min read

RAIS wa Amerika Joe Biden ameamua kumuunga Makamu wake Bi Kamala Harris kuwania Urais Novemba 2024 baada ya kusalimu amri ya kujiondoa kutetea kiti hicho.

Rais Biden alitangaza kutupilia mbali azma hiyo akisema ni uamuzi bora zaidi kwa wanachama wa Democrats. Alisema uamuzi huo, utamwezesha kutekeleza majukumu yake ya urais katika muhula wake uliosalia.

“Nimeamua kutokubali kuteuliwa na kuelekeza nguvu zangu zote katika majukumu yangu ya urais kwa muda uliosalia wa muhula wangu,” aliandika Bw Biden.

Rais huyo wa 46 katika nchi hiyo, alisema hatua hiyo ya kumuunga Bi Harris ilikuwa ni uamuzi wa kwanza aliofanya mwaka 2020 kama makamu wake.

“Ni uamuzi bora zaidi ambao nilifanya. Leo nataka kutoa uungwaji mkono na uidhinishaji wangu kamili kwa Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu. Wana Democrats, ni wakati wa kukusanyika na kumshinda Bw Trump. Hebu tufanye hivyo,” aliongeza Bw Biden.

Bw Biden aliandika barua kwa wananchi wa Amerika akiwashukuru kutokana na historia waliyoweka ya kuwekeza, kupunguza gharama ya dawa na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Tumetoa matunzo kwa mamilioni ya mashujaa walioathiriwa na vitu vyenye sumu…. Tulimteua mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika katika mahakama kuu na kupitisha sheria muhimu zaidi katika historia ya ulimwengu,” alisema Biden.

Rais huyo alishukuru kipindi ambacho alifanya kazi, akimpongeza makamu wake kwa kufanya kazi naye.