Ruto afuta ziara ya harambee katika shule ambako wazazi wanapunjwa
Na NDUNGU GACHANE
NAIBU Rais William Ruto, amefutilia mbali ziara ya Shule ya Upili ya Murang’a ambapo alitarajiwa kuongoza mchango Aprili 6, baada ya wazazi kulalamika kuwa wanalazimishwa kulipa Sh40,000 za ziada.
Harambee hiyo ililenga kuchangisha pesa za kujenga ukumbi, mabweni, madarasa, kituo cha teknolojia kilicho na maabara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na bwawa la kuogelea.
Mkuu wa shule hiyo, Bw Alex Kuria, alikuwa ameambia wazazi walipe pesa hizo kabla Aprili 6.
Mzazi ambaye aliomba asitajwe jina alisema wasimamizi wa shule hiyo walikuwa wanalazimisha wazazi kulipa pesa hizo kabla siku ya harambee ambayo ingesimamiwa na Bw Ruto.
“Awali tulikuwa tumeambiwa tuchangishe Sh50,000 lakini baadaye kiwango hicho kikapunguzwa kwa Sh10,000. Hatukushauriwa kuhusu suala hilo na tulikuwa tunalazimishwa tu, na hiyo si haki,” akasema.
Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata, alithibitisha Bw Ruto ameahirisha ziara hiyo lakini hakutoa sababu zake. “Ni kweli naibu rais amenijulisha hatazuru shule hiyo wiki hii lakini hakueleza kama msimamo wake umetokana na malalamishi ya wazazi kwamba wanalazimishwa kulipa pesa kwa harambee,” akasema.
Seneta huyo alisema Bw Ruto alipangiwa kuzuru Shule ya Upili ya Murang’a iliyo mjini Murang’a na Shule ya Upili ya Kiaraithe iliyo Kangema.
Taifa Leo ilibainisha kuwa wanachama ya Bodi ya Usimamizi wa shule hiyo na Chama cha Wazazi na Walimu walikutana kwa muda mrefu Alhamisi iliyopita kujadili hatua itakayochukuliwa kufuatia malalamishi ya wazazi na uamuzi wa Bw Ruto kutohudhuria harambee.
“Tulikuwa tunatarajia mchango mkubwa kutoka kwa naibu rais ambaye amekuwa akishiriki kwenye michango ya shule hii tangu mwaka wa 2015 lakini tunatumai atapanga kuwa nasi siku nyingine,” mmoja wa wanachama wa bodi hiyo akasema, na kuomba asitajwe.
Mkurugenzii wa Elimu katika Kaunti ya Murang’a, Bi Victoria Mulili, alisema maafisa kutoka kwa Wizara ya Elimu walichunguza kama shule ilifuata kanuni kabla kutoza wazazi pesa hizo, na uamuzi utatolewa hivi karibuni.
Kanuni huhitaji wasimamizi wa shule waandike barua kwa Bodi ya Elimu ya Kaunti kuomba ruhusa ya kutoza wazazi fedha.
Baada ya hapo, afisi ya mkurugenzi wa elimu katika kaunti hutakikana kuwasilisha ombi hilo kwa Waziri wa Elimu ambaye ndiye huamua kama ni sawa wazazi kutozwa ada zozote.
Mbali na hayo, wazazi ambao watoto wao walikamilisha masomo katika shule hiyo pia walilalamika kuwa watoto wao wamenyimwa vyeti vyao vya kukamilisha elimu ya sekondari kwa kuwa hawajalipa Sh40,000 zilizotakikana.
“Tulikuwa tumefanya harambee mwaka uliopita tukaambiwa na mwalimu mkuu tulipe Sh40,000 ambazo siwezi kugharamia. Cheti cha mwanangu bado kimekwama. Anahitajika kujiunga na chuo kikuu,” akasema mzazi.