Habari Mseto

Sonko, Badi warushiana tope kuhusu taka mitaani

November 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

UHASAMA kati ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya jiji la Nairobi (NMS), Meja Jemedari Mohammed Badi, unaendelea kuchacha huku wawili hao wakilaumiana kuhusu utupaji wa taka katika mitaa ya jiji.

Kuanzia Jumapili, wawili hao wamekuwa wakirushiana maneno baada ya Bw Sonko kushambulia NMS kwa kushindwa kuzoa taka zinazorundikana katika mitaa ya jiji.

“Supa gavana wa Nairobi ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Kenya na amiri jeshi mkuu wa majeshi Uhuru Muigai Kenyatta na Saddam Hussein wanafanya kazi ya ziada Pipeline eneobunge la Embakasi Kusini. Endeleeni na kazi bomba,” Bw Sonko alikejeli kwenye ujumbe aliochapisha katika ukurasa wake wa Facebook.

Hata hivyo, ofisi ya Meja Jemedari Badi ilimlaumu kwa kulipa watu kuhujumu utendakazi wa NMS kwa kumwaga milima ya taka jijini.

“Huku wakiendeleza hujuma zao kwa kumwaga rundo za taka, NMS na wakazi wa Nairobi wanaotambua jukumu lao la kudumisha usafi wa mazingira wanaendelea na kazi kila siku wakikusanya na kuzoa tani 3000 tofauti na kilo chache zilizokuwa zikizolewa awali,” NMS ilisema kwenye ujumbe Jumatatu.

Shirika hilo lilimlaumu Bw Sonko kwa ongezeko la taka jijini kwa kukosa kulipa wanakandarasi na kuvuruga juhudi za kusafisha jiji kwa kukatalia kandarasi zao.Hii imefanya wanakandarasi hao kugoma na kulazimisha NMS kutegemea Vijana wa Huduma ya Taifa (NYS) na malori yao kuzoa taka.

“Tuligundua kwamba taka zilimwagwa katika maeneo kadhaa ambayo tulikuwa tumesafisha. Serikali ya jiji pia imekwamilia kandarasi za wazoaji taka na kufanya NMS kuwafikia,” ilisema taarifa ya shirika hilo.

“Hizi ni siasa tu. Hatuwezi kulipa wanakandarasi kwa sababu serikali ya kaunti imekataa kutukabidhi mikataba yao ili tuweze kuzungumza nao na kuwalipa. Hata hivyo, tuko mbioni kusajili wanakandarasi wetu,” taarifa hiyo ilieleza.

Hata hivyo, Bw Sonko alisema kwamba NMS inafaa kubeba msalaba wake na kukoma kumtumia kama kisingizio cha kushindwa kuhudumia wakazi wa Nairobi.Kupitia msemaji wake Ben Mulwa, Bw Sonko alisema uzoaji wa taka ni jukumu la NMS lakini shirika hilo limeshindwa kudumisha usafi jijini.