Walimu watisha kugoma wakiendelea kuhamishwa
Na BARACK ODUOR
WALIMU wametishia kugoma muhula ujao kama serikali haitabadilisha sera za kuhamisha walimu kutoka maeneo yao ya kijamii.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Bw Wilson Sossion, alisema wanataka pia serikali ifutilie mbali mtindo wa kutathmini utendakazi wa walimu na badala yake walimu wawe wakipandishwa vyeo kwa msingi wa kisomo chao.
Akizungumza katika Shule ya Upili ya Homa Bay wakati wa mkutano wa mwaka wa Knut katika tawi hilo Jumapili, Bw Sossion alisema masuala hayo yanaathiri vibaya utendakazi wa walimu.
Akiandamana na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga, aliipatia serikali siku 20 kuanzia leo kutimiza matakwa ya walimu.
“Hakuna shule itafunguliwa kwa muhula wa pili kama serikali haitatimiza mahitaji haya. Tutaitisha mgomo mkubwa humu nchini kuanzia siku ya kufungua shule,” akasema.
Kulingana naye, mgomo utaanzishwa na walimu ambao watapiga kambi katika afisi za Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).
Bw Sossion alilalamika kuwa sera ya kuhamisha walimu kutoka maeneo yao ya kijamii itaathiri utendakazi wao kwani ndoa za wengi zitatatizwa.
“Hatua hii itavunja familia za walimu wengi wakihamishwa hadi maeneo yaliyo mbali na nyumbani kwao,” akasema.
Msimamo wake uliungwa mkono na Bi Wanga ambaye alisema hatua hiyo ya serikali itadhuru jamii za walimu husika.
Kulingana naye, walimu wanaofunza katika maeneo yao ya kijamii huwa wanategemewa kutoa aina zingine za usaidizi kwa jamii.
Alilaumu TSC kwa kupuuza wito wa kupandisha walimu vyeo wanapokamilisha elimu ya juu licha ya walimu kutumia rasilimali zao kuendeleza masomo.
“Inasikitisha kuwa walimu wengi walijitahidi kwa kutumia fedha kidogo kuendeleza elimu yao lakini TSC inasema itapuuzilia mbali vyeti vyao vya elimu kufanya uamuzi wa kuwapandisha vyeo,” akasema Bi Wanga.
Bw Sossion alisisitiza kuwa walimu walioendeleza masomo yao lazima wapandishwe vyeo.