Ruto, Gachagua kupimana nguvu katika uchaguzi wa UDA Mlima Kenya
RAIS William Ruto wiki hii anakabiliwa na kivuli cha kisiasa cha aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, huku chama chake cha UDA kikijiandaa kufanya chaguzi za mashinani katika eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Chama tawala kinatarajiwa kuendesha chaguzi hizo Jumamosi katika ngome zake za Mlima Kenya na Bonde la Ufa, shughuli inayotarajiwa kuwa kipimo cha mwelekeo wa kisiasa na inayoweza kubadilisha miungano ya kisiasa.
Maeneo haya mawili yalikuwa nguzo muhimu katika ushindi wa Rais Ruto mwaka wa 2022, lakini Mlima Kenya sasa unaonekana kuyumba baada ya kuondolewa kwa Bw Gachagua madarakani kupitia Bunge mnamo Oktoba 2024.
Bw Gachagua amekuwa akisisitiza kuwa eneo hilo lilimtaliki kisiasa Rais Ruto baada yake kumng’oa mamlakani kama naibu rais.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA, Bw Anthony Mwaura, alisema chama kinatarajia ushindani mkali kutokana na hamu kubwa ya wanachama wanaowania nyadhifa mbalimbali.
Alisema kuwa UDA ililazimika kuongeza muda wa usajili mara mbili ili kutoa nafasi kwa wote wanaotaka kushiriki.
Awali, usajili ulikuwa ufungwe Desemba 23, 2025, ukaahirishwa hadi Desemba 31, kisha Januari 5, 2026.
Kufikia Desemba 23, takriban wanachama 100,000 walikuwa wamejitokeza kuwania nyadhifa za ngazi ya vituo vya kupigia kura.
Katika kila kituo cha kupigia kura, wanachama watapiga kura kuwachagua maafisa 20. Kulingana na mwongozo wa chama uitwao Mwongozo wa Uchaguzi Mashinani, uchaguzi utahusisha wawakilishi watatu wa makundi ya kidini, wanne wa wafanyabiashara, watatu wa wataalamu, wanne wa vijana, mwakilishi mmoja wa Makundi Maalum ya Kijamii, wawakilishi watatu wa wakulima na wanachama wawili wa chama (mwanamke na mwanaume).
Bw Mwaura alisema jumla ya makarani 24,000 wa uchaguzi, maafisa wasimamizi 12,000 na polisi 24,000 watahusika kusimamia zoezi hilo.
Chaguzi zitafanyika katika kaunti za Embu, Kiambu, Kirinyaga, Laikipia, Meru, Murang’a, Nyandarua, Nyeri na Tharaka Nithi. Katika Bonde la Ufa, UDA itafanya chaguzi katika kaunti za Baringo, Bomet, Elgeyo Marakwet, Kericho, Nakuru, Nandi, Trans Nzoia, Uasin Gishu na Samburu.
Katika eneo la Magharibu mwa Kenya chaguzi zitafanyika Kakamega na Vihiga.
Chaguzi za Mlima Kenya zinatarajiwa kuwa mtihani mgumu wa umaarufu wa Rais Ruto, huku baadhi ya washirika wake wa karibu wakionekana kumuunga mkono Bw Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP).
Viongozi kadhaa wa UDA wanaotajwa kuwa wamejitenga na Rais Ruto ni pamoja na Ndindi Nyoro, John Methu, Joe Nyutu, Karungo Thang’wa, Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk, James Gakuya, James Murango na John Kinyua. Katika kaunti ya Kakamega, Seneta Boni Khalwale pia ametofautiana na Rais baada ya kuondolewa kama Kiranja wa Wengi katika Seneti.
UDA inapanga kufanya Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) Aprili 2026 kuchagua viongozi wa kitaifa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kampeni za Rais Ruto za kuwania muhula wa pili.