Jiandaeni kwa wiki ya baridi kali, upepo na mvua kiasi, Idara yashauri Wakenya
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imewataka Wakenya katika maeneo mbalimbali kujiandaa kwa mvua, baridi kali na upepo mkali wiki hii.
Katika utabiri wake wa hivi karibuni kwa wiki hadi Julai 18, idara hiyo ilisema kuwa maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Viktoria, Bonde la Ufa na maeneo ya Kaskazini-Magharibi mwa Kenya yanatarajiwa kuendelea kupokea mvua.
Aidha, maeneo ya Pwani yanatarajiwa kukumbwa na upepo mkali wa kutoka kusini na kusini-mashariki.
Wakazi wa kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi wanatarajiwa kupata vipindi vya jua asubuhi kwa sehemu kubwa ya wiki, isipokuwa Ijumaa na Jumamosi ambapo mvua za asubuhi zinatarajiwa kunyesha katika baadhi ya maeneo.
Maeneo haya pia yanatarajiwa kupokea mvua ya hapa na pale wakati wa alasiri na usiku kwa muda wa wiki nzima. Joto la juu zaidi katika maeneo haya linatarajiwa kuwa nyuzi joto 26 kwa kipimo cha selsiasi.
Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta, pamoja na maeneo ya ndani ya kaunti ya Tana River, yanatarajiwa kuwa na jua mchana na hali ya mawingu usiku wiki hii.
Kulingana na idara ya hali ya hewa, maeneo haya yatakuwa na joto la juu la nyuzi joto31 kwa kipimo cha selsiasi na la chini zaidi la nyuzi joto 12.
Kwa upande mwingine, wakazi wa kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, na maeneo ya pwani ya Tana River wanatarajiwa kupokea mvua ya hapa na pale kwa muda wa wiki nzima, isipokuwa Jumanne asubuhi, Alhamisi asubuhi na alasiri, Ijumaa na Jumamosi alasiri ambapo kutakuwa na hali ya jua.
Maeneo haya ya Pwani yatakuwa na joto la juu la nyuzi joto 30 kwa kipimo cha Selsais na la chini la nyuzi 21..
Mvua mchana kutwa ikifuatana na ngurumo za radi inatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, na West Pokot kwa siku tano zijazo.
Idara ilisema kwamba joto la juu katika kipindi hiki linatarajiwa kufikia nyuzi joto 30 kwa kipimo cha selsiasi, huku la chini likiwa nyuzi joto 10.
Kaunti za Turkana na Samburu zinatarajiwa kushuhudia mvua na manyunyu wakati wa mchana na usiku kwa wiki nzima. Wakazi wa maeneo haya watakumbwa na joto la juu la nyuzi joto 35 na la chini la nyuzi 11 kwa kipimo cha selsiasi.
Hali ya juu ya joto katika kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo inatarajiwa kuwa nyuzi joto 36 huku ya chini ikiwa nyuzi joto 14 kwa kipimo cha selsiasi.