Viongozi wa ODM, UDA wampangia Gachagua Magharibi, Bonde la Ufa
VIONGOZI wa ODM na wale wa UDA kutoka ukanda wa Magharibi na Bonde la Ufa, wamebashiri kuwa, chama kipya cha DCP kilichozinduliwa wiki hii hakitapenya kwenye ngome zao kuelekea 2027 huku wakikitaja kama cha kikabila.
DCP inaongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na ilizinduliwa rasmi Alhamisi wiki hii katika mtaa wa Lavington.
Kwenye hotuba yake wakati wa uzinduzi huo, Bw Gachagua alisema DCP inasimamia mabadiliko nchini na itashirikiana na vyama vingine kuhakikisha Rais William Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
Jana, wabunge wa ODM na UDA kutoka Magharibi na Msaidizi wa Rais William Ruto, Bw Farouk Kibet, walisema chama hicho hakitakuwa na ushawishi wowote Magharibi na Bondeni kutokana na ushirikiano kati ya vyama hivyo viwili.
Wabunge Mary Emase (Teso Kaskazini), Bernard Shinali (Ikolomani), Beatrice Adagala (Mbunge Mwakilishi wa Kike Vihiga) na Chistopher Aseka wa Khwisero, wakiongea eneobunge la Ikolomani, Kakamega, waliahidi kuwa DCP haitavuma Magharibi.
Wengine ambao walihudhuria mkutano huo na kumwaambia Bw Gachagua asahau uungwaji mkono kutoka ngome za ODM na UDA ni Mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe, Geoffrey Mulanya (Nambale) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda.
Aliyekuwa Seneta wa Kakamega na Katibu wa UDA Cleophas Malala aliteuliwa naibu kiongozi wa DCP katika hafla ya Alhamisi jijini Nairobi.
Bw Aseka alisema aliyekuwa naibu rais alitelekeza Magharibi wakati alikuwa mamlakani kwa kuwa alikuwa akilenga tu maendeleo ya Mlima Kenya pekee.
“Gachagua alitangaza kuwa serikali ilikuwa ya hisa na waliompigia Rais Ruto kura 2022 ndio wangenufaika kisha wengine wapewe makombo. Alikuwa na nia ya kuzuia maendeleo isifike Magharibi akisema tulimchagua Raila Odinga,” akasema Bw Aseka.
Bw Mugabe naye alisema utawala wa Kenya Kwanza unalenga kufungua kiuchumi eneo la Magharibi kupitia ujenzi wa Barabara Kuu ya Nairobi-Kampala ambayo itapitia kaunti za Kakamega, Bungoma na Busia.
Pia, alisema reli ya kisasa ya SGR ambayo ipo mpangoni kujengwa, itapitia Vihiga, Kakamega na Busia.
“Eneo la Magharibi limekuwa likinyimwa maendeleo kwa muda mrefu na ni serikali hii inafufua matumaini yetu ya kupata maendeleo,” akasema Bw Mugabe
“Kama watu wa Magharibi, tunaunga mkono ushirikiano wa Rais na kiongozi wetu Raila Odinga ili watu wetu nao wanufaike kwa miradi ya maendeleo,” akaongeza.
Kwa Bi Emase, nia yao kama viongozi ni kutokomeza umaskini badala ya kujihusisha na siasa za mgawanyiko ambazo alisema ni dhahiri zitaendelezwa na DCP.
Bw Kibet alisema Bw Gachagua aliondolewa mamlakani kutokana na siasa za kikabila na sasa ameunda chama kipya kuendeleza ajenda yake.
“Hicho chama hakina mwelekeo na hata wakati wa uzinduzi wake uliona jinsi waliyohutubu walikuwa wakipambana kueleza falsafa yake. Chama cha kikabila hakina nafasi nchini wakati Rais Ruto analenga kuwaleta Wakenya pamoja,” akasema Bw Kibet.
Bw Gachagua yumo kwenye muungano na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa PLP aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I na Eugene Wamalwa wa DAP-K.