Kimataifa

Mataifa yakemea Rwanda waasi wa M23 wakiendelea kuingia jijini Goma, DRC

Na REUTERS January 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GOMA, DRC, CONGO

MATAIFA mbalimbali sasa yanakemea Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoendelea kuingia kwa wingi katika mji mkuu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Umoja wa Mataifa ulikemea hatua ya wanajeshi wa kawaida wa Rwanda kuliunga mkono kundi hilo la waasi.

Naye Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alisema kwamba AU inafuatilia kwa makini matukio yote mashariki mwa DRC.

Viongozi mbalimbali akiwemo Rais William Ruto wa Kenya pia amesema atasimama na rais wa DRC, Felix Tshisekedi.

Haya yalijiri siku moja tu baada ya kundi hilo kusema limetwaa mji wa Goma na kuwaamuru wanajeshi wajisalimishe kufikia saa tisa alfajiri.

Corneille Nangaa, kiongozi wa Muungano wa Mto Congo unaojumuisha M23, aliambia Reuters kwamba vikosi vyake vilidhibiti mji huo.

Siku ya Jumatatu jioni, Waziri wa Maendeleo ya Vijijini Muhindo Nzangi alisema jeshi la Congo lilidhibiti asilimia 80 ya Goma, huku wanajeshi wa Rwanda wakiwa kwenye viunga vya mji huo.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la taifa la Congo Vital Kamerhe, alisema tathmini ya kijeshi inaonyesha kuwa wanajeshi wa serikali na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali bado wanadhibiti maeneo fulani.

Alisema Rais Felix Tshisekedi atalihutubia taifa kuhusu suala hilo, bila kutoa tarehe.

Lakini afisa mwingine wa Congo, ambaye aliomba kutotajwa jina, alisema waasi walitwaa asilimia 90 ya Goma.

M23 ilisema mapema Jumatatu kwamba imechukua udhibiti wa ofisi za shirika la utangazaji la taifa la Congo huko Goma, na wafanyakazi wawili wa huko wakathibitisha habari hiyo.

Katika kikao kilichofanyika New York, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, Bruno Lemarquis, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mapigano yanaendelea na kwamba hakuna aliye salama.

“Kuna wanajeshi wa Rwanda Goma wanaounga mkono M23,” mkuu wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix aliwaambia waandishi wa habari.

Mkazi mmoja wa Goma aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa aliwaona wanaume waliovalia sare za jeshi la Rwanda siku ya Jumatatu.

“Mnamo saa kumi na mbili jioni, nilitoka nje ili (kuona) hali ilivyokuwa. Niliona askari wakiwa wamevalia sare mpya kabisa za Rwanda,” mkazi wa Goma ya kati alisema.

Greg Ramm, mkurugenzi wa nchi wa shirika la kibinadamu la Save the Children nchini Congo, alisema, “Dakika chache tutaripoti kwamba vitongoji viko shwari. Dakika chache baadaye, tunasikia ripoti za mashambulio mapya ya makombora.”

Mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano ya hivi majuzi au vita vya awali wamekuwa wakiishi Goma na katika kambi zilizo karibu.

Kuwasili kwa waasi wa M23 katika mji huo kutawafanya maelfu kupoteza makazi yao na kusabababisha mgogoro wa kibinadamu.