Habari

Osotsi: Tutatalikiana na UDA ikiwa hatutapata majibu kuhusu mauaji ya Ojwang’

Na CHARLES WASONGA June 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi sasa anatisha kuwa chama hicho kitavunja “ndoa” yake na chama cha UDA ikiwa maafisa wa polisi wanaodaiwa kumuua mwanablogu Albert Ojwang’ hawatafutwa kazi na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Akiongea Jumanne, Juni 10, 2025 katika ukumbi wa seneti, Seneta wa Vihiga haswa alipendekeza kufutwa kazi kwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat aliyedaiwa kuamuru kukamatwa na Ojwang’.

Ilidaiwa kuwa Bw Lagat alikerwa na ujumbe ambao mwendazake aliweka kwenye mtandao wa kijamii na ambao ulimchagulia jina.

“Tulitia saini mkataba wa maelewano (MOU) na UDA na tukakubaliana kwamba visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela havitaruhusiwa kuendelea. Ikiwa hatutapata majibu kuhusu kifo cha Ojwang’ kutoka kwa serikali ya UDA, tutachukulia kuwa huo ni ukiukaji wa MOU yetu na UDA,” Bw Osotsi akasema.

“Kwa hivyo, hatutaona haja ya ushirikiano wetu kuendelea kudumu katika hali kama hii,” akasema Naibu huyo wa Kiongozi wa ODM.

Kauli ya Bw Osotsi alijiri baada kero kutanda nchini kufuatia kifo cha kutatanisha cha Bw Ojwang’ katika kituo cha polisi cha Central Nairobi usiku wa kuamkia Jumapili, Juni 8, 2025.

Kulingana na Bw Osotsi inasikitisha kuwa kifo cha Ojwang’ kinaonekana kama kuendelea kwa mtindo wa kunyamazishwa kwa wakosoaji wa serikali kwa kuwatishwa, kuteswa na hata kuuawa.

“Taifa hili limeshuhudia hali kama hii miaka ya nyuma na hatuwezi kuivumilia tena chini ya Serikali hii Jumuishi,” Seneta huyo wa Vihiga akasema.

Bw Osotsi pia alishutumu Msemaji wa Polisi kwa kutoa taarifa Jumatatu kwamba kifo cha Ojwang’ kilitokana na kujigonga kwake kwenye ukuta wa seli alikozuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central Nairobi.

Kauli kali ya Bw Osotsi ilijiri saa chache baada ya bosi wake Raila Odinga kutaka serikali itoe maelezo kuhusu ni nani aliamuru Ojwang akamatwe.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri huyu Mkuu wa zamani alitaka maafisa waliomkamata Ojwang nyumbani kwao Homa Bay Jumamosi wiki jana watambuliwe.

“Ojwang’ sasa anajiunga katika orodha ya vijana ambao maisha yao yamekatizwa katika njia ya kikatili, mikononi mwa polisi,” akasema.

“Inasikitisha kuwa sasa raia hawajui kutofautisha kati ya ukatili wa polisi na ukatili wa umma. Ni kana kwamba taifa hili limefeli kabisa,” Bw Odinga akaeleza.