Habari Mseto

Hatutaki ahadi za Ruto, wakazi wa Magharibi wasema wakihimiza viwanda vifufuliwe

Na SHABAN MAKOKHA August 21st, 2024 1 min read

KUNDI la wakazi katika eneo la Magharibi limepuuzilia mbali ahadi za Rais William Ruto kuhusu miradi ya maendeleo na badala yake kuirai serikali kufufua viwanda vilivyoporomoka eneo hilo kabla ya kuendeleza mipango mingine.

Wakazi hao ambao wameathirika baada ya viwanda maarufu kuporomoka ikiwemo Kampuni za Sukari ya Mumias na Nzoia, Kiwanda cha Pamba cha Busia, wamelalamika kuwa wamegeuzwa ombaomba huku vijana wakishiriki uhalifu ili kujikimu kimaisha, serikali ikiendelea kutoa ahadi tele.

Wamekosoa uzinduzi wa mradi wa maji wa Sh2 bilioni katika kaunti ndogo ya Malava wakisema eneo hilo limejaaliwa maji tele kutoka mitoni, chemichemi na visima.

Haya yamejiri siku moja baada ya Rais Ruto kuongoza hafla ya kuzindua rasmi mradi wa maji Malava Lot III, katika kijiji cha Namanja, kaunti ndogo ya Malava, Jumamosi.

“Katika eneo la Magharibi, hatuhitaji msaada wa maji. Tuna maji kwa wingi. Tatizo letu kuu ni kuhusu nafasi za kazi kwa vijana na hela mifukoni mwetu. Serikali inapaswa kuzindua viwanda vipya ikiwa wanahisi hawawezi kufufua vilivyoporomoka,” alisema Yusuf Odipo, mkazi wa Shisisia, Mumias.