Mke wangu alianza pombe polepole sasa ni mlevi chakari, nimsaidie vipi?
Mpendwa shangazi,
Huu ni mwaka wa tano tangu tuoane na mke wangu.
Uhusiano wetu umekuwa mzuri lakini mapema mwaka huu alianza kujihusisha na ulevi.
Alianza pole pole wakati wa wikendi lakini sasa amezidi kiwango cha kuwa analewa kila siku.
Nimsaidiaje?
Anachohitaji mkeo ni ushauri nasaha na apelekwe katika kituo rasmi cha kurekebishia tabia.
Mama mkwe hana adabu kabisa, anapita hadi chumba cha kulala!
Shikamoo shangazi?
Nimeoa mke kutoka jamii nyingine ambapo nimeona mambo ya kushangaza.
Kinyume na utamaduni wetu ambapo mama mkwe anapaswa kuwa na heshima zake, huyu wa kwangu amekosa adabu kabisa.
Kwanza anatutembelea kila siku na kuingia hadi katika chumba chetu cha kulala. Kuna wakati ambapo hata anakaa kwenye kitanda chetu.
Kwetu huo ni mwiko. Jamaa zangu wakijua wanaweza kukasirishwa na hata kushinikiza nimtaliki mke wangu. Nimkanyeje?
Katika jamii nyingi za Kiafrika hilo halikubaliki. Kaa na mkeo na umwambie azungumze na mamake kuhusu mipaka.
Simpendi lakini anajipendekeza sana kwangu!
Hujambo shangazi?
Kuna binti mmoja ambaye amekuwa akijipendekeza kwangu lakini simtaki. Nilimleta kwangu mara moja ambapo tulishiriki tendo la ndoa, na tokea siku hiyo amekuwa akija kila wikendi, kunifulia na kunipikia. Nimwambieje simtaki?
Sijambo!
Wajua kwamba wewe mwenyewe ulimuongoza kudhani kwamba ulikuwa unampenda. Kwa sasa huna budi ila kumwambia ukweli kabla ya mambo kuharibika zaidi.
Bosi wangu wa kike anataka nimzalishe, nimuamini?
Mpendwa shangazi,
Mimi ni mwanamume wa miaka 40. Kazini ninakofanya kazi kuna bosi mmoja wa kike ambaye amekuwa akinimezea mate.
Anasema ananitamani kutokana na utanashati wangu na kwamba angetaka nimzalishe, huku akiahidi kwamba hatonifuata na majukumu baadaye.
Nimuamini?
Kuzaa na mtu ni agano na ikiwa wewe mwenyewe hauna hiari ya kufanya hivyo, usithubutu. Pia, kwa sasa anaweza kukuambia kwamba hatokuelekezea jukumu lolote kuhusiana na mtoto, lakini una uhakika upi kwamba hatageuka baadaye?