Makala

UREMBO: Jinsi unavyoweza kuitunza ngozi yako

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KUNA vyakula vingi vya asili ambavyo ndani yake vimesheheni virutubisho muhimu vinavyosaidia mwili kupambana na magonjwa na kuimarisha afya ya ngozi. 

Miongoni mwa vyakula hivyo ni pamoja na vile vyenye asili ya kijani ama majani na ambavyo huwa na uwezo mkubwa katika kuponya magonjwa na kusaidia kujenga kinga ya mwili.

Sehemu kubwa ya miili yetu ni ngozi na ni sehemu muhimu ambayo ina jukumu kubwa la kuukinga na kuufunika mwili na viungo mbalimbali; na hivyo afya yake pia ni vizuri ikizingatiwa.

Vyakula tunavyokula vinaweza kuchangia katika muonekano wa ngozi zetu na kusaidia kupambana na matatizo ya ngozi, ikiwa ni pamoja na kupunguza mikunjo ya uso na suala zima la afya na muonekano wa ngozi.

Kutokuwa na ufahamu sahihi wa namna ya kudumisha afya za ngozi zetu na kutofahamu njia sahihi za kudumisha afya za ngozi zetu huchangia kushindwa kufikia lengo na mara nyingine hujikuta tukijisababishia madhara ikiwemo kupata maradhi makubwa yasiyotibika aghalabu hapo baadaye.

Kila tunavyokula vyakula bora ndivyo ngozi zinavyoonekana vizuri.

Vyakula hivi vinaweza kusaidia kuimarisha afya ya ngozi

Asali

Asali ambayo hutengenezwa na nyuki kwa viambato asilia ni chakula muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya ngozi na pia afya ya binadamu.  Hii ni kwa sababu kila kilichokizuri katika afya yako ni kizuri pia kwa ngozi.

Kwa kawaida ngozi nzuri huhifadhi unyevunyevu ili kuzuia kukauka na kupasuka na ndio maana huwa tunatumia mafuta ili kuifanya ngozi iwe na unyevu.

Hivyo asali husaidia kutunza na kuhifadhi unyevu kwenye ngozi na ina kiwango kikubwa cha sukari na asidi ambazo huzuia vijidudu wanaozaliana kwenye ngozi.

Tumia asali kwa kupaka wakati wa kuoga, kisha acha kwa muda na ioshe. Kufanya hivyo husaidia kuinawirisha ngozi.

Mayai

Mayai pia ni muhimu kwa afya ya ngozi yako. Kiini cha yai huwa na vitamini A na B huku sehemu yenye ute ikiwa na protini nyingi ambayo ni muhimu pia kwa ngozi, ute wa yai ni muhimu katika kuifanya ngozi kuwa nyororo na yenye kung’aa na pia husaidia ngozi kujilinda vizuri na mionzi ya jua.

Limau

Limau ni muhimu katika kuimarisha afya ya ngozi, kwa sababu husaida kutengeneza collagen, ambayo ni aina ya protini inayotengeneza ngozi.

Vitamini C husaidia sana kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi na hivyo kuilinda ngozi isizeeke mapema.

Mboga za majani

Hizi pia ni muhimu kwa afya ya ngozi kwani kama tujuavyo zimesheheni vitamini na virutubisho vya aina mbalimbali vyenye faida kubwa kwa ngozi na mwili kwa ujumla.

Kama unataka uwe na ngozi nyororo, unapaswa kutosahau kula mboga hizi za majani kwani husaidia ngozi kuzalisha seli mpya na kuondoa zile zilizokufa, hivyo kupunguza ukavu na kutunza ngozi na kuifanya ing’are na kuvutia.

Vyakula vya baharini

Kwa ujumla, hivi ni vizuri kwa afya ya ngozi. Vyakula vingi vya baharini vina kiwango kikubwa cha Zinc na Omega 3 ambayo ni muhimu kwa siha ya ngozi.

Faida za Omega 3 ni pamoja na kuondoa kukakamaa au ukavu wa ngozi, kupunguza kuvimba na kukunjamana kwa ngozi na husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini hivyo kuboresha ngozi.

Fanya mazoea ya kupenda kula vyakula vyenye lishe bora kwa kuwa na ngozi bora zaidi.