Bambika

Makokha ‘Baby Face’ atafuta msaada wa kifedha kwa mazishi ya mkewe

June 6th, 2024 1 min read

NA MARGARET MAINA

MWIGIZAJI maarufu wa kipindi cha ‘Vioja Mahakamani’ Bw Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha, anaomba msaada wa kifedha ili kugharimia mazishi ya mkewe, ambaye aliaga dunia siku chache zilizopita.

Mbali na fedha hizo za mchango kusaidia katika maandalizi ya mazishi, pia zitatumika kwa kukamilisha bili ya matibabu ambayo mkewe alikuwa akipokea kabla ya kifo chake.

Taarifa ya ombi la jamaa, ndugu na marafiki kutoa mchango ilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya mipango ya mazishi, ambaye pia ni mwenzake wa muda mrefu katika uigizaji, Bw Hiram Mungai Ngigi almaarufu kama Ondiek Nyuka Kwota.

Kipindi cha Vioja Mahakamani hupeperushwa na kituo cha runinga cha KBC, ambacho kinamilikiwa na serikali.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nyuka Kwota alipakia picha za Makokha na mkewe, marehemu Purity Wambui. Ni picha ambazo wanandoa hao walipigwa pamoja wakati Purity alikuwa hai.

Nyuka Kwota alieleza kwamba marehemu aliacha bili kubwa ya hospitali ambayo Makokha anahitajika kulipa.

Familia ya Makokha inahitaji msaada huo marehemu Purity kuandaliwa mazishi mazuri na ya heshima.

“Tunawafikia nyinyi wakati wa shida. Mcheshi wetu mpendwa Matayo Msagani Keya, ambaye wengi wanamfahamu kama Makokha Makacha ‘Baby Face’, anapitia wakati mgumu. Mke wake mpendwa, Purity Wambui Msagani, aliaga dunia, na tunawaomba msaada wenu ambapo fedha zitasadia kukamilisha bili ya hospitali na kumpa marehemu mazishi anayostahili,” akaandika Ondiek Nyuka Kwota.

“Ikiwa ungependa kumsaidia Matayo wakati huu mgumu, tafadhali tuma mchango kwenye akaunti ifuatayo: Nambari ya Akaunti/Mpesa: 7870966. Jina la Akaunti: Shanice Njeri Msagani. Ukarimu wako na upendo wako unathaminiwa sana,” Nyuka Kwota akasihi.

Siku tatu zilizopita, Nyuka Kwota alijulisha umma kuhusu kifo cha mkewe Makokha kupitia mitandao ya kijamii, ambacho kilisababisha mshangao mkubwa kwa wengi.

Hata hivyo, tangazo halikutoa maelezo ya kina kuhusu chanzo halisi cha kifo hicho.

[email protected]