Michezo

Harambee Stars yanusurika na sare dhidi ya Gambia

Na CECIL ODONGO March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Harambee Stars Alhamisi usiku ilitoka nyuma mara tatu na kuandikisha sare ya 3-3 dhidi ya Gambia kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia iliyogaragazwa Cote d’Ivoire.

Kenya ilikuwa ikivaana na Gambia katika mechi ya kundi F iliyochezwa kwenye uga wenye uwezo wa kusitiri mashabiki 60,000 wa Alassane Quattara jijini Abidjan.

Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha mpya wa Harambee Stars Benni McCarthy tangu arithi mikoba kutoka kwa Engin Firat mnamo Machi 3, 2025.

Winga Musa Barrow alifungia Gambia inayofundishwa na kocha wa zamani wa Gor Mahia Johnathan McKinstry mabao mawili dakika za 60 na 84 baada ya winga wa Brighton Yankuba Minten kuwapa uongozi dakika ya 54.

Nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga alifunga mkwaju wa penalti dakika ya 67 huku Mohamed Bajaber akiongeza bao jingine dakika ya 75.

William Lenkupae ambaye pia aliingia kipindi cha pili, alifungia Kenya bao dakika ya mwisho muda wa ziada kuzuia Stars kupigwa. Bao hilo lilisherehekewa sana na benchi ya kiufundi ya Stars.

Sare hiyo bado imeiwacha Kenya katika nafasi ya nne kwa alama sita baada ya mechi tano huku Gambia ikiwa ya tano kwa alama nne baada ya idadi sawa ya mechi.

Gabon ambayo iliichapa Ushelisheli 3-0 inaongoza kundi hilo kwa alama 12 baada ya mechi tano. Inafuatwa na Cote d’Ivore ambayo inachapana na Burundi mnamo Ijumaa kwa alama 10 huku Ushelisheli ikiwa haina alama yoyote.

Harambee Stars inatarajiwa kurejea nchini Ijumaa jioni kuenda kambini huku wakijiandaa kuvaana na Gabon kwenye mechi nyingine ya kundi F mnamo Jumapili katika uga wa kitaifa wa Nyayo.

Hii itakuwa mara ya kwanza ambapo Kenya itakuwa ikicheza nyumbani baada ya miaka miwili. Kenya imekuwa ikiandaa mechi zake Uganda na Afrika Kusini kutokana na ukosefu wa uwanja wakati ambapo nyuga zilikuwa zikiendelea kukarabatiwa kwa ajili ya CHAN itakayofanyika mnamo Julai.

Mshindi wa Kundi F atafuzu Kombe la Dunia litakaloandaliwa Canada, Mexico na Amerika.