Michezo

Kasarani kuandaa goli la Mashemeji baada ya kutotumikwa kwa siku 607

Na CECIL ODONGO May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UGA wa Kasarani ambao unaweza kuwasitiri mashabiki 60,000 utakuwa mwenyeji wa Debi ya Mashemeji Jumapili hii huku Shirikisho la Soka nchini (FKF) Jumanne likitoa onyo kali kwa Gor Mahia na AFC Leopards dhidi ya kuzua fujo katika mechi hiyo ya Ligi Kuu (KPL).

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kasarani kutumiwa kuandaa mechi tangu Septemba 12, 2023, Kenya ilipolazwa na Sudan Kusini bao 1-0.
Uwanja huo ulifungwa ili ufanyiwe ukarabati baada ya mechi hiyo wala haujawahi kuwa mwenyeji wa mechi kwa kuwa ukarabati bado unaendelea kwa ajili ya dimba la Mabingwa wa Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN).
Kenya na jirani zake Uganda na Tanzania,  itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya Agosti 2025.
Pia uga wa Kasarani umekuwa ukifanyiwa ukarabati kwa ajili ya mechi za Kombe la Afrika (AFCON) ambazo zitaandaliwa na mataifa hayo ya Afrika Mashariki mwaka wa 2027.
“Kasarani itakuwa mwenyeji wa Debi ya Mashemeji wikendi hii na shirikisho limehusishwa katika mipango ya mchuano ambao wenyeji ni Gor Mahia.
“Tunalenga sana usalama wa mashabiki, wasimamizi wa mechi na wote ambao watakuwa ugani humo,” akasema Katibu wa FKF Harold Ndege kwenye kikao cha jana.
“Hatutaki kile ambacho kilifanyika Gusii kirudiwe na mashabiki wa timu zote mbili, lazima wahakikishe wanaonyesha viwango vya juu vya nidhamu. Wale ambao wanazua ghasia watakabiliwa vilivyo,” akaongeza.
Jana, maafisa wa Gor Mahia walikutana na Ndege na wenzao wa AFC Leopards kuimarisha maandalizi kwa mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki wengi na huenda ikaamua mshindi wa taji la KPL msimu huu.
Kasarani iliandaa Mashemeji Derby mnamo Januari 29, 2023 ambayo iliishia sare tasa kati ya timu hizo mbili. Halaiki ya mashabiki walihudhuria.
Debi ya Mashemeji wikendi hii itakuwa ya 97 kati ya Gor na Ingwe.
Mechi ya mkondo wa kwanza Nyayo mnamo Machi 30 iliisha kwa sare tasa lakini pia ikagubikwa na fujo. Mashabiki walivunja lango na kuingia kwa lazima.
Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya Ingwe na K’Ogalo ilistahili kusakatwa Novemba 23 mwaka jana lakini ikaahirishwa kwa sababu Ingwe haikuwa na uwanja kwa kuwa Nyayo na Kasarani zilikuwa zimefungwa kufanyiwa ukarabati. Mechi hiyo iliahirishwa hadi Machi 1 lakini tena ikasongeshwa mbele hadi Machi 30. Mechi ya mkondo wa pili ilifaa kusakatwa Aprili 6 lakini ikaahirishwa.