Habari za Kitaifa

ODM inatuhangaisha, Kalonzo, Wamalwa sasa walia

Na JUSTUS OCHIENG August 22nd, 2024 2 min read

VYAMA tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya vinalia kudhulumiwa na ODM japo vinasisitiza kuwa vitasalia katika muungano huo.

Vyama hivyo vilianza kutoa lalama hizo baada ya ODM kukubali wanachama wake watano washirikishwe katika baraza la mawaziri la Rais William Ruto huku ikiendelea kukwamilia nafasi za uongozi bungeni.

Hatua hiyo sasa imesababisha mgawanyiko mkubwa katika muungano huo huku vinara wa Azimio wakionyesha kutokuwa na imani na uongozi wa kinara wao Raila Odinga.

Lakini chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga kimegeuka tena na kulaumu washirika wake kwa kusababisha migawanyiko ndani ya muungano huo kwa kuendeleza malalalamishi kuhusu hatua ya Rais Ruto kuteua wanachama wake serikalini.

Chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Wiper kinachoongozwa na Bw Musyoka sasa vimeungana na DAP-K, PNU na Kanu kujaribu kumwondoa Bw Odinga kama kiongozi wa Azimio.

Lakini sasa juhudi zao zinaonekana kugonga mwamba kwa sababu ODM inaonekana kutumia wingi wake kusambaratisha juhudi zao.

Baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Azimio kutibuka Jumatatu, Agosti 19, 2024, ODM sasa imetishia kuwapokonya wanachama wa vyama hivyo nafasi zao katika Kamati za Bunge la Kitaifa na Seneti endapo vitaendelea kumshambulia Bw Odinga.

Naibu kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi Jumatano, Agosti 21, 2024 alionya kwa kuwa wao ndio nambari mbili kwa wingi katika mabunge yote mawili, wanaweza kutwaa nafasi za kamati “ikiwa wenzetu wataendeleza vita”.

Bw Osotsi ambaye ni Seneta wa Vihiga alionya kuwa jaribio lolote kufurusha ODM katika Azimio ‘litawagharimu’ wenzao katika vyama shirika.

“Hii ni kwa sababu ODM ndicho chama kikubwa miongoni mwa vyama vya upinzani kwa mujibu wa idadi ya wanachama wake katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

“Ninawashauri kusoma na kuelewa sheria za mabunge yote mawili na watagundua kuwa tunaweza kuwaondoa na wanachama wetu ndio watashikilia nafasi zote katika kamati,” Bw Osotsi akaeleza.

Wakati huu, ODM inashikilia nafasi za Kiongozi wa Wachache kupitia Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na Kiranja wa Wachache kupitia Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.

Naibu Kiongozi wa Wachache ni Mbunge wa Kathiani Robert Mbui (Wiper) na Naibu Kiranja wa Wachache ni Mark Mwenye (Mbunge wa Embakasi Magharibi, Jubilee).

Katika Seneti, Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo (ODM) ndiye Kiongozi wa Wachache, huku Naibu wake akiwa Enoch Wambua (Seneta wa Kitui, Wiper).

Seneta wa Narok, Ledama Ole Kina (ODM) ndiye Kiranja wa Wachache huku naibu wake akiwa mwenzake wa Nairobi Edwin Sifuna (ODM).