• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Italia kukosa fainali za Kombe la Dunia 2022 baada ya kuduwazwa na Macedonia ya Kaskazini kwenye mchujo

Italia kukosa fainali za Kombe la Dunia 2022 baada ya kuduwazwa na Macedonia ya Kaskazini kwenye mchujo

Na MASHIRIKA

MABINGWA wa Euro 2020, Italia, hawatashiriki Kombe la Dunia mnamo 2022 baada ya kudenguliwa na Macedonia ya Kaskazini kwenye nusu-fainali ya mchujo mnamo Alhamisi mjini Palermo.

Aleksandar Trajkovski alifungia Macedonia ya Kaskazini bao hilo la pekee na la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa.

Kichapo hicho kinamaanisha kwamba Italia kwa sasa watakosa kunogesha fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo. Sasa watalazimika kusubiri kwa angalau miaka 12 kabla ya kujaribu tena bahati yao ya kushiriki kipute hicho kitakachoandaliwa kwa pamoja na Mexico, Amerika na Canada mnamo 2026.

Ni miezi minane pekee imepita tangu kocha Roberto Mancini aongoze Italia kukomoa Uingereza ugani Wembley na kunyanyua taji la Euro 2020.

Italia walikamilisha kampeni zao za makundi katika nafasi ya pili nyuma ya Uswisi baada ya kushinda mechi nne na kuambulia sare mara nne.

Licha ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kutamalaki mchezo kwa muda mrefu, Italia walilenga shabaha langoni mwa Macedonia Kaskazini wanaoorodheshwa nambari 67 duniani mara tano pekee licha ya kuelekeza makombora 32.

Macedonia Kaskazini kwa sasa wako pua na mdomo kufuzu kwa fainali za haiba kubwa katika ulingo wa soka kwa mara ya pili mfululizo baada ya kunogesha fainali za Euro 2020. Italia ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia, kwa sasa wanashikilia nambari sita duniani kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa matusi mitandaoni

DOMO: Kheri msela na Kizungu chake cha kuboronga!

T L