• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Ramsey apachika wavuni mabao mawili na kusaidia Wales kupepeta Belarus

Ramsey apachika wavuni mabao mawili na kusaidia Wales kupepeta Belarus

Na MASHIRIKA

WALES walipepeta Belarus 5-1 ugani Cardiff City na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye Kundi E kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Mchuano huo ulikuwa wa 100 kwa nyota Gareth Bale kutandaza ndani ya jezi za timu ya taifa ya Wales. Bao la Aaron Ramsey liliwaweka Wales kifua mbele katika dakika ya pili kabla ya Bale kuchangia goli la pili lililojazwa kimiani na Neco Williams aliyemwacha hoi kipa Sergei Chernik wa Belarus.

Bale aliyekuwa akiwajibikia Wales kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kuuguza jeraha kwa miezi miwili iliyopita aliondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Ramsey alifanya mambo kuwa 3-0 alipofunga penalti katika dakika ya 50.

Ben Davies alifunga bao lake la kwanza kimataifa na kufanya mambo kuwa 4-0 katika dakika ya 77. Baada ya Artem Kontsevoi kufungia Belarus katika dakika ya 87, Connor Roberts alizamisha kabisa chombo cha wageni wao dakika moja kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Wales kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi E kwa alama 11, tatu zaidi kuliko nambari tatu Jamhuri ya Czech watakaovaana na Estonia mnamo Novemba 16, 2021. Licha ya ushindi huo mnono dhidi ya Belarus, matumaini ya Wales kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia moja kwa moja yalizimika rasmi baada ya Ubelgiji kuwacharaza Estonia 3-1.

Wales tayari wamefuzu kwa mchujo wa kuwania tiketi ya kuelekea Qatar baada ya kuibuka washindi wa Kundi lao kwenye Nations League mwaka uliopita wa 2020. Hata hivyo, watalazimika kukamilisha kampeni za Kundi E katika nafasi ya pili ili wasakate mchuano ujao wa mchujo mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Sare ya aina yoyote dhidi ya Ubelgiji mnamo Novemba 16, itawaweka Wales wanaonolewa na kocha Robert Page katika ulazima wa kukamilisha kampeni za Kundi E katika nafasi ya pili. Afueni zaidi kwa Wales ni kwamba wameshinda mechi mbili kati ya tatu zilizopita dhidi ya Ubelgiji wanaoshikilia nafasi ya kwanza duniani kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA).

You can share this post!

Argentina pua na mdomo kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya...

Ubelgiji wakomoa Estonia na kuingia Kombe la Dunia 2022...

T L