Kimataifa

Trump sasa ahubiri umoja baada ya kunusurika kifo wikendi

Na MASHIRIKA July 15th, 2024 1 min read

MILWAUKEE, AMERIKA

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump Jumatatu alihimiza umoja akiwa katika mji wa Milwaukee alikoenda kufanya matayarisho ya mwisho kabla ya uteuzi wake rasmi kama mgombeaji urais wa chama cha Republican, siku mbili baada ya kunusurika kifo.

Hii ni baada ya kushambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa sikioni mjini Butler, jimboni Pennsylvania na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20.

Trump, 78, alikuwa akiendesha kampeni katika uwanja wa Bethel Park, aliposhambuliwa na kijana huyo kwa jina Thomas Mathew Crooks.

Crooks, alimpiga risasi Trump kwa kutumia bunduki aina ya AR-15.

Mshukiwa huyo aliyetekeleza uhalifu huo akiwa amepanda juu ya paa la jengo moja aliuawa papo hapo na maafisa wa usalama.

Hata hiyo, Rais huyo wa zamani hakujeruhiwa vibaya zaidi, kwani alitibiwa na akaendelea na shughuli zake.

“Ukweli umeanza kuonekana,” Trump akaambia gazeti la Washington Examiner Jumatatu.

“Hata hivyo, huu ni wakati wa kupalilia umoja nchini Amerika, hata ni wakati wa kuleta umoja duniani,” akasema baada ya kuwasili mjini Milwaukee.

Akaongeza: “Ni nadra kwangu kutoangalia umati wa watu ninaowahutubia. Endapo singefanya hivyo wakati huo (Jumamosi), hatungekuwa tukiongea leo, tungeongea kweli?”akauliza.

Mbali na Crooks, mtu mwingine aliuawa na wengine wawili wakajeruhiwa katika umati huo.

Katika hutoba zao Jumapili Trump na Rais Joe Biden walihimiza utulivu na umoja, wakilenga kupunguza joto la kisiasa na uhasama nchini Amerika.

Biden alitoa hotuba yake kutoka Oval Office katika Ikulu ya White House.

“Uhalifu wa aina hiyo hauwezi kuruhusiwa kutendeka Amerika. Hatuwezi kuruhusu hali kama hii kushuhudiwa nchini,” akasema.

“Joto la kisiasa limepanda zaidi nchini. Linapasa kupungua mara moja,” Rais Biden akasema kwenye hotuba hiyo iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.