Bambika

Ucheshi wa Morey wamuacha Waiguru hoi taabani

June 5th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MNAMO Juni 1, 2024, wakati wa sherehe za Madaraka Dei, mcheshi Francis Mwaganu Murage almaarufu Morey Wakibiru alimuacha Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru hoi taabani akiangua kicheko.

Bw Mwaganu aliwajibikia nafasi yake kwa dakika zaidi ya 10 na bado Bi Waiguru akionekana kukataa watu wa itifaki kumwondoa jukwaani, akiomba mistari ya ucheshi izidi kuporomoshwa na kijana huyo.

Sio tu pua la Waiguru ambalo lilikuwa katika hatari ya kukatika, bali pua za waliokuwa katika ukumbi wa sherehe hizo zilijipata katika hatari sawa.

Bi Waiguru alionekana mara kwa mara akiwa katika safari ya kuokotwa chini akicheka bila breki, huku pia akipanguza machozi ya furaha kutoka macho yake.

Ucheshi wa kijana huyu wa umri wa miaka 31 umekuja kujipa nembo ya kiwango cha kipekee ambapo hata busara ya kuhepa mitego ya kisiasa katika jukwaa kubwa la kisiasa ilijiangazia.

Huku akimtania Waiguru kwa kuwa mrembo ajabu kama kinyago, Bw Mwaganu alielezea jinsi ambavyo angependa kuandamana na Bi Waiguru katika ziara zake za kikazi katika mataifa ya ng’ambo.

“Lakini Gavana wetu mrembo si kupenda kwangu eti niliogopa tuandamane kwa kuwa mimi huvaa mitumba isipokuwa tu koti. Huwa nahofia tusiandamane nawe ughaibuni halafu tukutane na wenye nguo hizi zangu waniamrishe kuzitoa na ubaki na mzee aliyevalia koti pekee katika ujumbe wako,” akasema Bw Murage.

Nguo nyingi za mutumba huwa zinaagizwa kutoka Ulaya na Amerika baada ya wenyewe kuchoka nazo na kuzitupa.

Aidha alisema kwamba haoni haja ya kuandamana na Waiguru katika ziara za miji ya Ulaya kwa kuwa miji hiyo bado iko katika Kaunti ya Kirinyaga.

“Mnaenda kutembea nchini Paraguay na huku kwetu tuko na mji wa Baragwi. Mkienda mjini Massachusetts na huku kwetu tuko na Mucakuthi… mnaenda Michigan na huku tuko na Gichugu,” akasema.

Bw Mwaganu aliongeza kwamba mwaka wa 2027 Bi Waiguru akiondoka kitini baada ya kuhudumu awamu mbili za ujumla wa miaka 10 kutahitajika mrithi.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru akiangua kicheko. PICHA | MWANGI MUIRURI

Huku waliokuweko wakitega masikio kwa tamaa ya kupata dokezi, wakitarajia mcheshi huyo amtaje mwanasiasa mmoja kati ya wale ambao wanadadisiwa kuwa mfaafu, alisema: “Mimi ndio Waiguru atawachia”.

Bw Mwaganu alisema yeye aliokoka mwaka wa 1976 lakini Shetani akapaa angani kuomba ruhusa ya kumhangaisha.

“Shetani amekuwa akinihangaisha kiasi kwamba aliniulia ng’ombe wangu punde tu mnunuzi aliyekuwa ameingia kwa boma kumnunua alipowasili,” akasema.

Bw Mwaganu alisema “ukiwa mrithi wa Gavana Waiguru kazi itakuwa rahisi sana kwa kuwa “ukiwa umejenga hizi hospitali zote, siwezi nikalemewa na kazi rahisi ya kusema wagonjwa wapewe Panadol”.

Pia, alisema serikali ya Waiguru ikiwa tayari imeshirikisha kujengwa kwa bwawa la Thiba, kazi ya kufungulia maji ni mboga kwa mrithi wake.

“Hata hivyo hata useme ni mimi mrithi wako na uchaguzi uandaliwe Kwa wakati huu, Niko na uhakika wa asilimia 100 kwamba (Waiguru akaelekeza kidole kwa mcheshi ishara ya kukubaliana naye kwamba itakuwa ni yeye) nitaanguka,” akasema Bw Murage huku ukumbi wote ukiachwa hoi ukimchekelea Bi Waiguru kwa kuongozwa hadi kwa mtego wa kunoa utabiri.

Bw Mwaganu aliongeza kwamba “hata niko na maono kwamba Waiguru ataishia kuwa Rais wa Taifa hili na manifesto itakuwa ya watu wa Kirinyaga”.

Alisema wahudumu wa bodaboda wangependekeza serikali ya Waiguru iwe ikikubali wakamue mafuta ya magari ya polisi kwa kuwa huwa yamenunuliwa kwa kutumia ushuru wao.

“Pia, kadi ya bima ya afya ya NHIF iwe ikitumika kujinunulia vitamu kama pombe ya makali kwa walio na shida za tumbo,” akasema.

Bw Mwaganu alimtaka Bi Waiguru akishafika ikulu aifanye sheria vijana wapewe pesa yao ya wazee “wakizeeka watajipanga” na pia “wimbo wa Taifa uwe kwa lugha ya Kirinyaga” na bila kusahau kwamba “pale ambapo husemwa ndio upate wako wa maisha ni lazima uwabusu vyura 1,000 uvipunguze hadi vinne”.

Aliongeza kwamba siku ya Mwaka Mpya iwe maalum ambapo mifereji ya maji ya Kaunti iwe ikisambaza pombe na hata kwa kanisa misa ya Sakrameni iwe waumini wakipewa pombe aina ya Keg.

Bw Mwaganu alizidi kuporomosha mistari ya ucheshi huku ukumbi ukibakia kuchangamka ajabu.

Kile wengi hawafahamu ni kwamba alimpoteza babake mzazi mnamo Aprili 11, 2002.

Alisema dunia yake iligeuka kuwa ya kujituma akiwa na lengo la kukwepa msiba huo.

“Kwa wakati huo, singeelewa yaliyokuwa yamenifanyikia katika uthabiti wangu wa maisha. Lakini leo hii huo msiba hunigonga ndani ya moyo wangu huku nikibakia na ulezi wa mamangu pekee,” akasema.

Bw Mwaganu alisema kwamba imekuwa safari ya kuafikia viwango vya kutambulika hata na washirikishi wa hafla za hadhi.

“Haijakuwa rahisi. Ni safari ndefu na ngumu na Mungu amekuwa mwema kwangu kwa kunijalia kupendwa na maneno yangu yakikumbatiwa kwa kicheko na mashabiki wangu,” akasema.

Mcheshi Francis Mwaganu Murage almaarufu Morey Wakibiru. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alisema safari yake licha ya kuonekana kama imemfikisha kileleni, mashabiki wafahamu ndio tu imeanza.

“Tuendako ni mbali kuliko tutokako na tuliko. Tutapaa hadi kwa majukwaa ya kimataifa,” akasema.

Alimshukuru Bi Waiguru kwa “kuwa mlezi wa vipaji na ambaye alinipa moyo sana kumwona akifurahia kwa dhati kipaji changu kiasi cha kunituza na kunitambua hadharani kupitia kupigwa picha pamoja jukwaani wageni wote wa hadhi wakishuhudia”.

“Nilistaajabu Bi Waiguru kusimamisha Madaraka Dei kwa muda ili kunitambua na kupigwa picha nami. Hii inaonyesha miujiza ya Mungu,” akasema msanii huyo.

Mashabiki wa mcheshi Francis Mwaganu Murage almaarufu Morey Wakibiru wakiangua kicheko. PICHA | MWANGI MUIRURI