Habari za Kitaifa

Vigogo wa ODM hatarini kutolewa tonge mdomoni uteuzi wao serikalini ukipingwa kortini

Na MWANDISHI WETU July 26th, 2024 2 min read

UTEUZI wa viongozi wakuu wa chama cha upinzani ODM kwa nyadhifa za uwaziri sasa unaning’inia hewani kufuatia mwanaharakati mmoja kukimbilia mahakamani kupinga zoezi hilo.

Mwanaharakati Julius Ogogoh ambaye amefikisha kesi kortini. Picha|Maktaba

Mwanaharakati Julius Ogogoh amefikisha ombi kortini Ijumaa akitaka uteuzi wa Hassan Joho (kwa Wizara ya Madini na Uchumi wa Baharini), John Mbadi (Wizara ya Fedha), Wycliffe Oparanya (Wizara ya Vyama vya Ushirika) na Opiyo Wandayi (Wizara ya Kawi) uvunjiliwe mbali, akidai kwamba haukufuata katiba.

Bw Ogogoh, kupitia Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu, amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu akiitaka izuie Bunge la Kitaifa kuwapiga msasa Joho, Oparanya, Mbadi na Wandayi ili wateuliwe rasmi kuhudumu kama mawaziri.

Bw Ogogoh anasema Kenya inazingatia demokrasia ya vyama vingi na mbunge hawezi kujiunga na chama kingine baada ya uchaguzi.

Aidha, anasema kuwa uteuzi wa wanne hao utadhoofisha upinzani ndani ya bunge na kuhujumu utendakazi wa bunge kama asasi ya kuhakiki utendakazi wa serikali kuu.

“Endapo mwanachama wa mshtakiwa wa kwanza (Azimio) atateuliwa kuwa waziri upinzani ndani ya bunge utadhoofishwa hali ambayo ni kinyume cha Kipengele cha 75 cha Katiba,” akasema.

Mabw Oparanya na Joho ni manaibu wa Bw Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM ilhali Bw Mbadi ni mwenyekiti wa chama hicho.

Naye Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa Ugunja, ni Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa na Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika ODM.

Majina yao yamewasilishwa kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambaye ameweka tangazo magazetini akiomba umma kuwasilisha memoranda kuhusu ufaafu wa mawaziri hao wateule.

Lakini Bw Ogogoh anataka mahakama kuu ibatilishe uteuzi wa wanne kwa misingi kuwa umefanywa kinyume cha katiba.

Ameorodhesha muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, chama cha ODM, Bw Wetang’ula na Mwanasheria Mkuu kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Kupitia wakili, Nicholas Kamwenda, Bw Ogogoh anasema wanne hao ni wanachama wa Azimio na hivyo hawawezi kuteuliwa kuhudumu kama mawaziri.

“Kwa kuwa upinzani katika Bunge la Kitaifa una wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha utendakazi wa Serikali Kuu na matawi mengine ya serikali, hautaweza kutekeleza wajibu huo ipasavyo ikiwa wabunge wa mrengo huo watateuliwa kuwa mawaziri,” akasema.

Bw Ogogoh anaeleza kuwa hatua hiyo inaenda kinyume na wajibu ambao Wakenya wanataraji utekelezwe na upinzani.

“Matokeo ya uteuzi wa wabunge wa upinzani kujiunga na serikali ni kwamba hakutakuwa na upinzani katika Bunge la Kitaifa. Hakutakuwa uhakikisha wa serikali na matawi mengine na hivyo hayatawajibika kwa raia wa Kenya wanaopasa kuhudumiwa,” akasema.

Kulingana na Ogogoh hatimaye maovu yataendelea serikalini na maafisa wake hawawajibika ipasavyo.