Habari za Kaunti

Waathiriwa wa mafuriko walala nje, waliobomolewa bado hawajapokea Sh10,000

Na SAMMY KIMATU July 10th, 2024 1 min read

FAMILIA kadhaa ambazo ni waathiriwa wa mafuriko katika mtaa wa mabanda Mathare jijini Nairobi bado hawana makao hadi leo baada ya nyumba zao kusombwa na maji na zingine kubomolewa na tingatinga ili kupisha njia ya mkondo wa maji mkabala wa mto Mathare kwa mwezi wa pili.

Hali sawia na hiyo inashuhudiwa katika mitaa ya mabanda ya Mukuru inayopatikana katika kaunti ya Starehe, Makadara na kaunti ndogo ya Embakasi Kusini, baada ya Operesheni ‘Bomoa Bomoa’ kulenga kuwahamisha watu walioishi karibu na mto Ngong.

Katika mtaa wa Mathare, familia kadhaa hulala ndani ya makanisa na kumbi, huku katika maeneo ya Mukuru, wengine wakitafuta hifadhi katika jumba moja lililowazi na lililotumika kuchemshia vyuma vya reli miaka ya tisini na kuachwa baada ya shughuli kusitishwa.

Wengine huwasha moto nyakati za usiku angalau kusukuma muda baada ya kukosa pa kulala.

Kinachowatamausha waathiriwa hao ni kwamba hawajapata hela zilizotolewa na rais William Ruto alizotangaza Sh10,000 zitakazolipwa waathiriwa ili kurahisisha kuhama kwao wakitafuta makao kwingineko.

Mtaa wa mabanda Nairobi. PICHA| SAMMY KIMATU

“Nilipoteza kila kitu wakati wa mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha mwezi Aprili/Mei. Baada ya hapo nyumba yangu ya kupanga ilibomolewa na serikali. Bado sijapokea Sh10,000 za rais Ruto alizotuahidi kabla ya nyumba zetu kubomolewa,” mwanamke wa miaka 45 aliyefadhaika aliambia Taifa Leo.

Inadaiwa kwamba katika afisi za wakuu wa tarafa, visa vya ufisadi vilikithiri zaidi huku wale wasiolengwa na kuathirika na mafuriko wala nyumba zao kubomolewa, wakifaidika kwa kupewa Sh10,000 ilhali mwathiriwa aliyepoteza mali yake kwa mafuriko na nyumba yake aliyopanga ikibomolewa akibaki kuteseka kwa kukosa pesa.

“Inatamausha kuona machifu wakiongoza tingatinga kutubomolea makao yetu. Nimepoteza mali yangu kwa mafuriko. Sina mahali pa kulala na sijalipwa Sh10,000 na serikali ilhali kuna wengine waliolipwa hela hizo wakiishi mbali na mto na wajukuu wao mashambani. Ni aibu iliyoje! mwanamke mlemavu aliyeathirika akasema.

[email protected]