Habari za Kitaifa

Ziara ya Nyanza yaanika siri baina ya Ruto, Raila

Na CHARLES WASONGA August 31st, 2024 2 min read

SASA ni wazi kwamba muafaka kati ya Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ulinuiwa kuweka mikakati ya kumwezesha Kiongozi wa Nchi kuhifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Hilo lilijitokeza wazi kwenye kauli za Dkt Ruto, na wandani wa Bw Odinga, katika ziara yake ya siku nne eneo la Luo-Nyanza.

Japo ziara hiyo, inayokamilika Jumamosi Agosti 31, 2024, ilidaiwa kuwa ya kuanzisha na kukagua miradi ya maendeleo, Rais Ruto hakuficha nia yake ya kuvutia ufuasi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Katika kila kituo alikohutubia wananchi katika kaunti za Migori, Homa Bay, Siaya na Kisumu, Dkt Ruto aliwakumbusha wananchi alivyowahi kumsaidia Bw Odinga na jinsi kiongozi huyo wa ODM alivyomsaidia mwezi Julai alipokabwa koo na maandamano ya vijana wa Gen-Z.

“Mnajua kwamba wakati mmoja nilikuwa sio to mshirika bali mtetezi wake sugu, na mnajua kuna wakati nilimsaidia, sasa ikiwa Baba (Raila) amerudisha mkono na kunisaidia kuna shida gani?”

Dkt Ruto akawaambia wakazi wa Homa Bay Alhamisi huku akishangiliwa kwa furaha.Mnamo Jumatano, akiwa mjini Migori, Rais Ruto alisema kuwa ukuruba wa kisiasa kati yake na Bw Odinga sio wa muda mfupi bali utadumu kwa kipindi kirefu.

“Hii ndiyo maana Baba alinipa watu wake nikawateua mawaziri ili tupalilie umoja wa Kenya tukisonga mbele.

Na ningependa kuwahakikishia kwamba tutatembea pamoja hata baada ya Baba kuenda Addis Ababa (Ethiopia) kupigania kiti kikubwa cha Umoja wa Afrika (AU) ambacho atakishinda,” akaeleza.

Wanachama wa ODM ambao Dkt Ruto aliwateua katika baraza lake la mawaziri ni John Mbadi (Waziri wa Fedha), Wycliffe Oparanya (Ustawi wa Vyama vya Ushirika), James Opiyo Wandayi (Kawi), Ali Hassan Joho (Uchimbaji Madini) na Beatrice Askul (Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki).

Kwa upande wao, wandani wa Bw Odinga wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga waliapa ‘kusimama’ na Rais Ruto hadi 2027.

“Mheshimiwa Rais tunasema asante sana kwa kuwateua wenzetu kutoka eneo hili kuwa mawaziri katika serikali yako na tutasimama nawe hadi 2027. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii mtu kutoka eneo hili ameshikilia cheo cha Waziri wa Fedha. Isitoshe, historia imeandikishwa nchini kwani Nyanza imetoa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke,” akasema gavana huyo wa Homa Bay akirejelea uteuzi wa Dorcas Oduor kuchukua nafasi ya Mwanasheria Mkuu iliyoshikiliwa na Justin Muturi kabla ya kuteuliwa Waziri wa Utumishi wa Umma.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Tom Mboya anamtaja Rais Ruto kuwa mwanasiasa mwerevu kwani amegeuza madhila, yaliyomzonga tangu Mei kuwa faida kwake.

“Kwanza, ni uhasama kati yake na naibu wake Rigathi Gachagua. Pili, ni maandamano ya vijana wa Gen-Z. Ameamua kumvuta Odinga upande wake, na kuunga mkono azma yake ya kiti cha AUC, na hivyo kufaulu kabisa kuyeyusha hatari iliyomkodolea macho kufuatia uasi kutoka kwa naibu wake na Gen-Z,” anasema Dkt Mboya.

Msomi huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno anabashiri kuwa kufikia 2027 ngome za Bw Odinga za Nyanza, Magharibi na Pwani, zitakuwa nyuma ya Rais Ruto.

“Hilo likitimia, Rais Ruto hatahitaji uungwaji mkono kutoka Mlima Kenya, ikizingatiwa kura za maeneo hayo matatu zinazidi kura za Mlima Kenya. Hii ndiyo maana baada ya kushirikisha wandani wa Odinga katika baraza lake la mawaziri, ameamua kufanya ziara katika maeneo hayo kutoa shukrani zake kupitia uzinduzi wa miradi ya maendeleo,” Dk Mboya anaeleza.