Wakazi wampa mbunge notisi ya kumvua wadhifa, Machakos
WAPIGA kura wa Eneobunge la Machakos wameanza mchakato wa kumvua wadhifa mbunge wao Caleb Mule huku washirika wa Rais William Ruto katika eneo la Ukambani wakikabiliwa na wakati mgumu kwa kuunga Mswada wa Fedha 2024.
Wakazi wawili wa Mji wa Machakos, Joseph Mutinda Thomas na Thomas Mutuku Wambua, wameanzisha mchakato wa kumtimua Bw Mule kwa kumjulisha mbunge huyo kuhusu nia yao ya kumvua wadhifa wake kwa mujibu wa Kifungu cha 104 cha katiba.
‘Tumeagizwa na wateja wetu kukuandikia kukufahamisha kwamba kulingana na Kifungu cha 104 cha katiba, wateja wetu wanakupatia notisi ya kukuondoa kama Mbunge wa Eneobunge la Machakos. Hii inatokana na kukosa kutii mwito wao wa kukataa Mswada wa Fedha wa 2024. Kwa hivyo, watakuwa wakitia saini ombi ili kukutimua,” inasema notisi iliyoandikwa Juni 24 kwa mbunge na wakili Daniel Mutinda.
Mbunge anayehudumu muhula wa kwanza kwa tiketi ya Chama cha Maendeleo Chap Chap (MCCP) ni miongoni mwa wabunge sita wanaoegemea upande wa Rais William Ruto katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni ambao wamejipata motoni kwa kuunga mkono Mswada tata wa Fedha 2024 ambao umerudishwa bungeni.