Habari Mseto

Hii imeenda na ninafurahia kuwa mama mkwe, Shusho asema baada ya bintiye kula yamini ya ndoa kisiri

Na WINNIE ONYANDO August 3rd, 2024 1 min read

MWANAMUZIKI staa wa nyimbo za injili kutoka Tanzania, Christina Shusho, amekiri kuwa anafurahia kuwa mama mkwe katika umri wake mdogo.

Akizungumza jana baada ya kuwasili nchini Kenya, mwimbaji huyo alisema kuwa japo alijuta hapo awali kuolewa akiwa na umri mdogo, sasa anajivunia kuwa mama mkwe.

“Najihisi vizuri kuwa mama mkwe katika umri mdogo sana. Niliomba harusi ya faragha, jambo ambalo binti yangu ataishi kukumbuka,” akasema nyota huyo wa nyimbo za injili kwa kukiri anatazamia sasa kuanza kuitwa nyanya.

“Nahisi kwamba nitakuwa na nguvu ya kucheza na wajukuu wangu sasa,” akaongeza.

Hii ni baada ya Bi Shusho kutangaza kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa binti yake amefanya harusi ya faragha.

“Dada Ode Mrs Willy. Maneno kwishaaaaa. My firstborn got married in an exclusive private ceremony. From today, call me mama mkwe. I Thank God for His faithfulness,” akaandika.

Harusi hiyo kulingana na Bi Shusho ilihudhuriwa na watu wachache mno.

“Tulifanya hivyo mradi tu kuwapa hao wawili (binti yangu na mumewe) kuwa na picha za kumbukumbu. Ilikuwa pia namna ya kuwapongeza na kuwaambia wamefanya jambo la maana sana,” akaongeza.

Bi Shusho ni mama wa watoto watatu na mara nyingi hapendi kuyaanika mambo yake ya kibinafsi mitandaoni.

Alivuma sana nchini Kenya baada ya kufyatua vibao vyake vya ‘Shusha Nyavu’ na ‘Zakayo’.