DimbaMakala

Tanzania, Uganda wafuzu AFCON 2025 huku Kenya ikiumiza nyasi bure

Na LABAAN SHABAAN November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TAIFA Stars ya Tanzania imefuzu kushiriki Kinyang’anyiro cha kandanda ya mataifa ya bara Afrika (AFCON 2025) huko Morocco.

Lakini Harambee Stars ya Kenya ilibanduliwa katika michuano ya kufuzu dimba hilo.

Nyota wa Kenya walishinda mechi moja, kutoka sare tatu na kunyukwa mara mbili katika kundi J ambapo Cameroon na Zimbabwe walifuzu huku Kenya na Namibia wakiambulia patupu.

Sasa mitandaoni kumewaka moto serikali ya Kenya ikilaumiwa kwa kukosa kuandaa nyuga faafu za kuwezesha Kenya kuchezea mechi za nyumbani humu nchini ili kushangiliwa na mashabiki.

Harambee Stars walicheza mechi za nyumbani (dhidi ya Ivory Coast na Burundi) kufuzu Kombe la Dunia nchini Malawi.

Timu ya taifa haikucheza mechi yake yoyote ya kufuzu nchini kutokana na ukosefu wa uwanja ulioidhinishwa na Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF).

Mechi za nyumbani za kufuzu AFCON dhidi ya Zimbabwe na Cameroon zilichezewa Uganda, huku mchuano dhidi ya Namibia ikisakatiwa Afrika Kusini.

“Ni aibu kushiriki mechi za nyumbani katika nchi nyingine kwa sababu Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) hutoa ratiba ya mechi miaka mitatu kabla ya michuano ya kufuzu kuanza. Ni aibu kwa shirikisho la kandanda Kenya (FKF) na si haki kwa mashabiki wa kambumbu,” alisema mshambulizi wa awali wa Harambee Stars Dennis Oliech wakati Kenya ilicheza dhidi ya Ivory Coast.

Msuva aliokoa Tanzania

Bao la Simon Msuva katika kipindi cha pili kiliwapa vijana wa Taifa Stars ushindi muhimu dhidi ya Guinea walipochuana katika Uga wa Kitaifa wa Benjamin Mkapa mnamo Jumanne.

Ushindi huu uliwahakikishia Tanzania nafasi ya pili katika kundi la H nyuma ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DR Congo).

Ilikuwa mechi ya kufa kupona na kwa hivyo Msuva alidhihirisha ukakamavu ambao uliwabandua Guinea na Ethiopia na kuzima nyota yao ya kwenda Morocco.

Kunako dakika ya 61, Msuva alifunga bao la kichwa kwa kuunganisha krosi aliyomiminiwa na mchezaji mwenza Mudathir Yahya.

Ni bao ambalo liliwachacharusha mashabiki wa Tanzania waliojaa pomoni uwanjani Benjamin Mkapa kushabikia vijana wao.

Taifa Stars itashiriki AFCON mara ya nne katika historia ya mashindano hayo na mara ya pili mfululizo.

 Uganda ilifuzu pia

Uganda ilihitimisha kampeni yake ya kufuzu AFCON kwa ushindi waliopigania kwa damu na jasho dhidi Congo mjini Brazzaville kwa kuondoka na ushindi wa 1 – 0.

Bao la Travis Mutyaba  lililoyumbisha wavu katika kipindi cha pili  liliwapa Uganda Cranes nafasi ya kusakata boli kule Morocco 2025.

Uganda wameibuka wa pili katika kundi la K nyuma ya Afrika Kusini huku DR Congo na Sudan Kusini wakizimiwa nyota ya kung’aa katika AFCON itakayogaragazwa mwaka ujao.