Taifa Leo na Kenya Yearbook kushirikiana kuwafaa wasomaji
Na JUMA NAMLOLA
KAMPUNI ya Nation Media Group imeingia kwa mkataba na Kenya Yearbook kuchapisha masuala muhimu ya uchumi kupitia gazeti la Taifa Leo.
Kupitia mpango huo, gazeti la Taifa Leo litakuwa likichapisha baadhi ya makala na habari kuhusu masuala ambayo huchapishwa kwa Kiingereza katika Kitabu cha Serikali cha Kenya Yearbook.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini mkataba huo katika jumba la Nation Centre Jumatano, Mkurugezi Mkuu wa Uhariri, Bw Mutuma Mathiu (pichani kulia), alisema mpango huo wa ushirikiano utakuwa wa manufaa zaidi kwa wanafunzi.
“Kwa kuwa gazeti la Taifa Leo lina soko kubwa shuleni, habari zitakazochapishwa humo zitawanufaisha wanafunzi wa shule za msingi na za upili,” akasema Bw Mathiu.
Alikuwa akizungumzia makala mbalimbali katika gazeti la Taifa Leo, kama vile Marudio ya Mitihani, Shindano la Insha, Mashairi, Uchambuzi wa Fasihi na kijarida cha “Elimu”.
Kupitia ushirikiano huo mpya, Taifa Leo itakuwa ikichapisha habari zilizo ndani ya Kenya Yearbook katika masuala kuwahusu wanasiasa maarufu walioweka msingi wa historia ya nchi hii.
Mengine ni ya kuwahusu wanawake mashuhuri, ambapo yatakuwa yakichapishwa kwenye kijarida cha “Pambo” kinachotokea kila Jumamosi huku yale ya wanasiasa yatakuwa kwenye “Jamvi” kila Jumapili.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Yearbook, Bw Edward Mwasi (pichani kushoto), alisema wameamua kuchapisha taarifa na makala yao katika Taifa Leo, ili kuwafikia Wakenya wengi zaidi.
“Katika Kenya Yearbook tunachapisha habari na makala muhimu kwa nchi hii lakini katika lugha ya Kiingereza. Tunafahamu nafasi muhimu ya Kiswahili. Mbali na kuwa ni lugha rasmi Kenya, pia ni lugha ya kimataifa.,” akasema.
Anaamini kupitia gazeti la Taifa Leo, mamilioni ya Wakenya watapata maelezo hayo kwa lugha inayozungumzwa na wengi.
“Bodi ya Kenya Yearbook imejitolea kuhakikisha kuwa masuala muhimu ya maendeleo kwenye Ruwaza ya Mwaka 2030, yanawafikia Wakenya wote kwa lugha nyepesi, kupitia ushirikiano huu na gazeti la Taifa Leo,” akasema.