Mume kumlipa mkewe fidia ya Sh0.5m kwa ‘mpango wa kando’ nyumbani
MWANAMKE aliyemfikisha mumewe wa miaka 30 mahakamani ameshinda fidia ya Sh500,000 baada ya kuthibitisha kuwa hatua ya mumewe kumleta mwanamke mwingine katika nyumba yao ya ndoa ilikiuka haki zake za kikatiba.
Jaji wa Mahakama Kuu, Alfred Mebeya aliamua kuwa mwanaume huyo, GOB, alikiuka utu wa mkewe, BAC, kwa kumleta mpenziwe, FC, katika nyumba yao ya ndoa iliyoko Kombewa, Kaunti ya Kisumu.
Mahakama iliamuru GOB na FC kumlipa BAC fidia hiyo na FC kuondoka katika nyumba hiyo ndani ya siku 14 baada ya hukumu kutolewa. Majina ya wahusika yalifupishwa ili kulinda utambulisho wa watoto wao watatu walio chini ya umri wa miaka 18, wanaoishi na mama yao.
BAC aliiambia mahakama kuwa alifunga ndoa ya Kikristo na GOB Machi 16, 1996, na kwamba walikuwa wakiishi katika nyumba yao ya ndoa tangu 2017. Alisema kuwa mnamo Mei 13, 2026, mumewe alimleta FC nyumbani bila kumshirikisha wala kupata idhini yake, kisha akamruhusu kuendelea kuishi hapo. BAC alisema hatua hiyo ilikiuka haki zake za utu, faragha, afya na kuishi kwa amani nyumbani, huku ikiathiri pia ustawi wa watoto wao.
Jaji Mebeya alisema kumlazimisha BAC kuishi na mwanamke mwengine katika nyumba ya ndoa kulimsababishia fedheha, msongo wa mawazo na migogoro ya mara kwa mara.
Mahakama ilibaini kuwa kisa hicho kilizidi kiwango cha kutokubaliana kwa kawaida kati ya wanandoa, kwa kuwa uwepo wa FC uliharibu amani nyumbani na kusababisha mabishano na mivutano ya mara kwa mara.
Jaji alisema Katiba inalinda utu wa kila mtu na inakataza kudhalilishwa. Pia alisisitiza kuwa haki ya makazi bora inajumuisha uwezo wa mtu kuishi nyumbani kwa amani.
BAC alisema hali hiyo ilisababisha maumivu ya kihisia, kukosa usingizi na wasiwasi. Ripoti ya daktari iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kuwa msongo wa mawazo ulikuwa ukiongeza matatizo yake ya kiafya.
Mahakama pia ilisema kuwa mmoja wa wanandoa hawezi kubadilisha kwa upande mmoja misingi ya ndoa ya mke mmoja kwa kumleta mtu wa tatu nyumbani bila mashauriano au idhini ya mwenzake.
Jaji alihitimisha kuwa mwenendo huo pia ulijumuisha ukatili wa nyumbani chini ya Sheria ya Kuzuia Ukatili wa Nyumbani.