Wakurugenzi, maafisa wakuu watendaji kukutana kujadili namna ya kuimarisha biashara
WAKURUGENZI wa kampuni mbalimbali, maafisa wakuu watendaji (CEO) na wamiliki wa biashara wanatarajiwa kukutana Nairobi Novemba 20, 2026, kujadili mikakati ya kukuza biashara, kuboresha biashara na kupata wateja wapya kupitia mitandao ya kibiashara.
Mkutano huo wa mwaka wa Directors Referral Network (DRN) utafanyika katika Windsor Golf Hotel and Country Club kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.
Rais wa DRN, Dolphine Okeyo, alisema mkutano huo utatoa fursa kwa viongozi wa biashara kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazokabili kampuni zao na kuanzisha ushirikiano unaoweza kufungua milango ya kibiashara.

Alisema mkutano huo hautakuwa tu wa kupiga gumzo, bali pia utalenga kutafuta suluhu kwa changamoto zinazokabili biashara kila siku.
“Tunakutana kutatua changamoto halisi tunazokabiliana nazo kila siku,” alisema Bi Okeyo.
Aliongeza kuwa mahusiano ya kibiashara yanaweza kusaidia kampuni kupata washirika, wateja na fursa ambazo zingekuwa vigumu kuzipata bila kutangamana na watu wanaofaa.
Mratibu wa tawi la Muthaiga la DRN, Doreen Bosibori,

alisema mkutano huo pia utawapa wakurugenzi fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao huku wakijifunza kutoka kwa viongozi wa sekta nyingine.
Alisema kupata wateja katika mazingira ya sasa ya biashara kunahitaji kujenga uaminifu na kutangamana na watu wanaoweza kusaidia kukuza kampuni.
“Biashara ni ngumu kupata. Huwezi tu kuingia katika chumba na kupata wateja. Kukutana, kufahamiana na kuelewana hurahisisha kuanzisha mikataba ya kibiashara,” alisema.
Mkurugenzi mkuu wa Explicit Risk, Audit and Data Ltd (ERAD), Steve Gathai, alisema kutangamana na watu wenye mamlaka ya kufanya maamuzi ni muhimu kwa kampuni zinazotafuta wateja na ushirikiano.
Alisema mikutano kama hiyo inaweza kuwaunganisha watoa huduma za ukaguzi wa hesabu, kodi, usimamizi wa hatari na kuzuia ulaghai na kampuni zinazohitaji huduma hizo.
“Unahitaji kukutana na watu wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Jukwaa hili linakupa nafasi ya kuwasiliana nao, na hilo linaweza kuleta tofauti kati ya biashara inayopitia changamoto na ile inayofanikiwa,” alisema Bw Gathai.
Washiriki pia wanatarajiwa kujadili mikakati ya kuongeza faida, kuboresha mtiririko wa fedha na kupata wateja, huku wakijifunza kutokana na uzoefu wa wajasiriamali waliofanikiwa.
Mkutano huo utahusisha wakurugenzi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo uongozi wa kampuni, rasilimali watu, teknolojia, utalii na ujasiriamali.
Wandaaji wanasema mwaliko uko wazi kwa wakurugenzi na maafisa wakuu watendaji, pamoja na mameneja na wawakilishi wengine wenye mamlaka ya kufanya maamuzi katika mashirika yao.
Ada ya ushiriki ilikuwa Sh7,000 kwa waliojisajili mapema kati ya Oktoba 1 na 31, huku ada ya kawaida ikiwa Sh10,000 kwa usajili wa kati ya Novemba 1 na 18.