Vizingiti vinavyokabili ODM ikiendea nusu mkate na UDA
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinaingia katika hatua muhimu ya hesabu zake za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, kikitaka kugawana mamlaka kwa usawa na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) katika muungano unaopendekezwa kumuunga mkono Rais William Ruto.
Hata hivyo, huku kiongozi wa ODM Oburu Oginga akisisitiza kuwa chama hicho kinastahili nusu ya mamlaka kwenye makubaliano na UDA, mgawanyiko wa ndani na kutokubaliana kuhusu ushirikiano na Ruto vinatishia kudhoofisha msimamo wake katika mazungumzo.
ODM inataka kuwa mshirika sawa na UDA badala ya kuwa chama kidogo katika muungano unaotawaliwa na chama cha rais. Lakini kutaka nusu ya mamlaka na kuhakikisha inapata mgao huo ni mambo mawili tofauti.
Oburu alieleza msimamo huo hadharani Juni 2026, akisema makubaliano yoyote ya kabla ya uchaguzi kati ya ODM na UDA lazima yazingatie kanuni ya kugawana mamlaka kwa asilimia 50 kwa kila upande.
“Tutakapounda makubaliano ya muungano na UDA, yatategemea mgao wa asilimia 50 kwa kila upande, jambo litakalotufanya kuwa imara zaidi. Hata urais tutaujadili; hatutaacha kiti chochote bila mazungumzo,” alisema Oburu.
Wakizungumza wakiwa Turkana wiki jana, viongozi wa ODM walioongozwa na Mwenyekiti Gladys Wanga walisisitiza kuwa lazima makubaliano ya UDA yakitwe kwa msingi wa kugawana mamlaka nusu kwa nusu.
Kauli hizo zinaashiria kuwa ODM haitaki mazungumzo yahusu nyadhifa za Baraza la Mawaziri pekee, bali pia urais na nafasi nyingine muhimu katika serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi.
Hata hivyo, chama hicho kinapaswa kuthibitisha kuwa kina uwezo wa kuhamisha uungwaji mkono wake wa kisiasa hadi kwenye kura, kudumisha umoja na kuhakikisha wafuasi wake wa jadi wanabaki pamoja.
Kifo cha Raila Odinga Oktoba 15, 2025, kiliondoa mwanasiasa aliyekuwa mhimili mkuu wa ODM katika mazungumzo ya kisiasa kwa miongo kadhaa.
Raila hakuwa tu kiongozi wa chama, bali pia alikuwa mhamasishaji wa wafuasi, mpatanishi wa makundi yaliyokinzana na mtu aliyekuwa na uwezo wa kuunganisha viongozi wenye misimamo tofauti.
Ushawishi wake ulitokana na uzoefu wa kushiriki chaguzi kadhaa, mtandao wa kisiasa aliojenga kwa miaka mingi na uwezo wa kujadiliana na washirika akiungwa mkono na maelfu ya wafuasi nyuma yake.
Oburu sasa amebeba jukumu la kukiongoza chama katika kipindi hicho cha mpito, lakini changamoto yake ni kuonyesha kuwa nguvu za ODM zinaweza kudumu hata bila mtu aliyeunganisha makundi mbalimbali.
ODM bado ina viongozi waliochaguliwa, mitandao ya kisiasa katika maeneo tofauti na utambulisho wa kitaifa uliojengwa kwa miaka mingi. Hata hivyo, rasilimali hizo zitakuwa na thamani katika mazungumzo iwapo chama kitaonyesha kuwa kinaweza kuendelea kuwa na umoja kuelekea 2027.
Mazungumzo ya ODM na UDA yalipiga hatua nyingine Agosti 2026, Ruto na Oburu walipotangaza timu za kushughulikia mfumo wa kugawana mamlaka na manifesto ya pamoja ya muungano unaopendekezwa kwa uchaguzi wa 2027.
Hatua hiyo ilionyesha kuwa mazungumzo hayahusu tena iwapo vyama hivyo vitashirikiana, bali masharti vitakayokubaliana na namna yatakavyotekelezwa.
Kwa ODM, madai ya kugawana serikali kwa asilimia 50 ni msimamo wa mazungumzo, ambao haijulikani ikiwa utakubaliwa na UDA.
Kulingana na viongozi wa chama hicho cha chungwa, usawa huo utahusu idadi ya mawaziri, nyadhifa kuu serikalini, uongozi wa Bunge, maeneo ya kuwania viti na kushiriki katika maamuzi muhimu ya serikali.
“Masuala hayo yanahitaji kujadiliwa tofauti kwa sababu kupata idadi sawa ya mawaziri hakumaanishi moja kwa moja kuwa vyama vina mamlaka sawa katika kufanya maamuzi,” asema mchanganuzi wa siasa Jimmy Opiyo.
Suala jingine ni kugawana maeneo ya kisiasa, maarufu kama zoning, ambapo vyama hukubaliana kutosimamisha wagombeaji wanaoshindana katika maeneo fulani.
ODM imetaka suala hilo liwe sehemu ya makubaliano, lakini UDA imeonyesha kutokuwa tayari kulikubali, kulingana na taarifa kuhusu mazungumzo ya vyama hivyo.
Urais nao ni suala nyeti zaidi. Oburu amesema haupaswi kuachwa nje ya mazungumzo, lakini muungano unaopendekezwa pia unalenga kumuunga mkono Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Hali hiyo inaibua swali muhimu: Je, ODM inajadili masharti ya kumuunga mkono Ruto au inataka muungano ambao utawezesha kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya uongozi wa nchi?
Opiyo anasema jibu litategemea masharti yatakayowekwa katika makubaliano ya mwisho.
Anasema kuibuka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi kulidhoofisha nguvu za ODM katika majadiliano.
“Mgawanyiko huu unaweza kudhoofisha uwezo wa ODM kuwasilisha msimamo mmoja katika mazungumzo na UDA.Changamoto ya ODM si kupata nafasi serikalini pekee, bali kuhakikisha kuwa makubaliano yatakayofikiwa yana manufaa kwa chama na wafuasi wake,” asema.
Kushiriki katika serikali kunaweza kupatia ODM nafasi ya kushawishi sera, kugawana nyadhifa za uongozi na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa.
ODM inapaswa pia kutofautisha maslahi ya viongozi binafsi na yale ya wananchi wanaoiunga mkono. Kupata nyadhifa serikalini kunaweza kuwa na thamani kwa viongozi, lakini chama kinahitaji kuwaeleza wananchi namna ushirikiano huo utakavyoboresha maisha yao, utawala na uwakilishi wa kisiasa.
“Takwa la kugawana serikali kwa asilimia 50 halitakuwa na nguvu bila ODM kuonyesha kuwa ina uungwaji mkono wa kutosha, inaweza kudumisha wapigakura wake na ina umuhimu wa kisiasa katika uchaguzi ujao,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Anasema mazungumzo hayo yanapatia ODM fursa ya kulinda ushawishi wake katika serikali ya kitaifa, lakini pia yana hatari ya chama kuishia kumuunga mkono Ruto bila kupata dhamana ya kutekelezwa kwa madai yake.