Joho, Mvurya wapambania kudhibiti Kwale
USHINDANI wa kuwania ugavana Kwale kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 unazidi kuonekana kama mchuano wa kisiasa kati ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho wa ODM, na mwenzake wa Michezo, Bw Salim Mvurya wa UDA.
Bw Mvurya anaongoza juhudi za kuhakikisha kaunti hiyo inasalia chini ya UDA huku Bw Joho akitangaza nia ya ODM kuendeleza ushawishi wake katika eneo la Pwani.
“Ni lazima tukifanye ODM kuwa imara tena. Hatuwezi kuruhusu vyama vingine kuchukua maeneo yaliyokuwa ya ODM,” alisema Bw Joho wakati wa mkutano wa hivi majuzi wa kisiasa Kwale.
Gavana Fatuma Achani, ambaye anatumikia muhula wake wa kwanza, anakabiliwa na ushindani mkali baada ya waliokuwa wakimezea mate tikiti ya ODM, Profesa Hamadi Boga na mfanyabiashara Lungazi Mangale, kuamua kuungana ili kumuunga mkono mmoja wao.
Wawili hao, walioibuka wa pili na wa tatu mtawalia katika uchaguzi wa 2022, wamehimizwa na viongozi wa mashinani kudumisha ushirikiano wao hadi uchaguzi utakapofanyika.
Viongozi wa ODM wameonya kuwa kuvunjika kwa muungano huo kunaweza kudhoofisha azma ya chama hicho ya kutwaa kiti cha ugavana.
Licha ya mikakati hiyo inayoendelea, Waziri Mvurya amewataka wapinzani wa Bi Achani kujiandaa kwa mchuano mkali unaofanana na uchaguzi mdogo wa Msambweni wa mwaka 2020.
Uchaguzi huo ulikuwa kipimo kikubwa cha ushawishi wa kisiasa kati yake na Waziri Joho, ambao wakati huo walikuwa magavana wa Kwale na Mombasa mtawalia.
Bw Joho aliunga mkono mgombeaji wa ODM Omar Boga, ambaye ni kaka mdogo wa Profesa Boga, huku Mvurya, aliyekuwa mwanachama wa ODM kabla ya kuhamia Jubilee, akiunga mkono mgombeaji huru Feisal Bader.
Bw Bader alikuwa akiungwa mkono na wanasiasa waliokuwa washirika wa Naibu Rais wa wakati huo, William Ruto.
Hatimaye, Bw Bader alimshinda Omar kwa kupata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za mpinzani wake, na hivyo kumpa Mvurya ushindi mkubwa wa kisiasa.
“Si siri kwamba rais wetu ni William Samoei Ruto, gavana wetu ni Fatuma Mohamed Achani, na mbunge wa eneo hili ni Feisal Bader. Walimdharau Feisal katika uchaguzi mdogo wa 2020 na wakaja hapa kwa nguvu zao zote, lakini tunawaambia kuwa wanaweza kupanga dhidi ya gavana, lakini atasalia kuwa gavana wa Kwale,” alisema Bw Mvurya katika mkutano wa kisiasa Msambweni.
Profesa Boga, ambaye aliwahi kuhudumu kama Katibu katika Wizara ya Kilimo wakati wa utawala wa Jubilee, aligombea ugavana mwaka wa 2022 kupitia tiketi ya ODM na kupata kura 53,972, na kushika nafasi ya pili nyuma ya Bi Achani, aliyeibuka mshindi kwa kura 59,674.
Bw Mangale, aliyewahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Kenya (KPA) kama mhandisi, aligombea kupitia chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kabla ya kujiunga na ODM baada ya chama hicho kusambaratika.
Hata hivyo, Gavana Achani ametetea rekodi yake ya uongozi akisema anatarajia kuchaguliwa tena kutokana na miradi ya maendeleo ambayo serikali yake imeanzisha.
“Viongozi wanapaswa kutathminiwa na kuchaguliwa tena kwa kuzingatia miradi yao ya maendeleo. Acheni siasa za chuki na uhasama. Kuna baadhi ya watu ambao hawana sera; wanachozungumzia kila mara ni Achani. Nitachaguliwa tena ili kuhudumu mihula yangu miwili,” alisema.