Pambo

SHERIA: Ni kosa kuishi kwenye ndoa isiyosajiliwa rasmi

Na Benson Matheka November 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

Ndoa si sherehe, pete wala kuishi pamoja chini ya paa moja. Ni muhimu kuhakikisha imefanywa kwa mujibu wa sheria na kusajiliwa ili kulinda haki za wanandoa na watoto wao.
Watu wengi huingia kwenye ndoa kwa kufanya sherehe za kifamilia, kidini au kimila, kisha kuendelea na maisha bila kuhakikisha kuwa ndoa hizo zimesajiliwa rasmi. Wengine huona usajili kama jambo la urasimu lisilo na umuhimu, mradi tu wamekubaliana kuishi pamoja kama mume na mke.
Lakini kupuuza hatua hii kunaweza kuibua matatizo makubwa wanandoa wanapofarakana, mmoja wao anapofariki au kunapozuka mzozo kuhusu urithi, mali na haki za mwenzi aliyebaki.
Sheria ya Ndoa ya Kenya ya mwaka 2014 inaweka wazi wajibu wa kusajili ndoa na kutambua aina mbalimbali za ndoa zinazoweza kufungwa nchini, zikiwemo za kiraia, Kikristo, Kiislamu, Kihindu na kitamaduni.
Hata hivyo, kufungwa kwa ndoa na kusajiliwa kwake ni hatua mbili ambazo hazipaswi kuchanganywa. Wanandoa wanapaswa kuhakikisha kuwa ndoa yao imeunganishwa na mtu aliyeidhinishwa na kwamba taratibu za kisheria za usajili zinafuatwa.
Kutosajili ndoa kunaweza kuhatarisha uhalali wake.
Sehemu ya 42 ya Sheria ya Ndoa inaelekeza mtu anayefungisha au kusimamia ndoa kuwasilisha nakala ya cheti cha ndoa kwa Msajili wa Ndoa ili maelezo yake yaingizwe katika sajili rasmi.
Sheria hiyo pia inaweka adhabu kwa mtu anayeshindwa kusajili ndoa. Akipatikana na hatia, anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh5,000.
Jambo muhimu zaidi ni kwamba sehemu ya 12 ya sheria hiyo inasema ndoa inaweza kubatilishwa ikikosa kusajiliwa rasmi. Hii ina maana kuwa wanandoa hawapaswi kudhani kuwa sherehe waliyoifanya pekee inatosha kuwahakikishia ulinzi kamili wa kisheria.
Katiba ya Kenya, katika Ibara ya 45, inatambua familia kama msingi wa jamii na kuipa ulinzi wa Serikali. Pia inahakikisha kuwa wanandoa wana haki sawa wakati wa kufunga ndoa, wanapoishi pamoja na ndoa inapovunjika.
Haki hizo zinapaswa kuambatana na kufuata taratibu za kisheria ili kuepusha hali ambapo mmoja wa wanandoa analazimika kutumia muda na fedha nyingi kuthibitisha uhusiano wake.
Ndoa za kitamaduni hazijaachwa nyuma.
Baadhi ya Wakenya hudhani kuwa ndoa za kimila hazihitaji kusajiliwa kwa sababu zinatambuliwa na wazee na familia za wahusika.
Lakini Sheria ya Ndoa imeweka utaratibu maalumu kwa ndoa hizo kusajiliwa. Sehemu ya 44 inataka wahusika kuarifu Ofisi ya Msajili wa Ndoa ndani ya miezi mitatu baada ya kukamilisha taratibu na sherehe zinazotambulisha muungano wao chini ya mila husika.
Aidha, sehemu ya 55 inawataka wanandoa kuwasilisha maombi ya cheti cha ndoa ndani ya miezi sita baada ya kukamilisha taratibu za kimila. Wote wawili wanapaswa kufika mbele ya Msajili ili kukamilisha usajili.
Hivyo basi, kulipa mahari, kufanya sherehe ya kitamaduni na kutambuliwa na wazazi au wazee wa jamii hakupaswi kuwa mwisho wa safari. Hatua za usajili ni muhimu pia.
Wanandoa wanaoishi nje ya nchi pia wanapaswa kuchukua tahadhari.
Sheria haijawasahau Wakenya wanaofunga ndoa nje ya nchi. Sehemu ya 39 inaruhusu Wakenya kufunga ndoa za kiraia katika balozi za Kenya katika mataifa ya kigeni, mradi masharti yaliyowekwa yatimizwe.
Aidha, sehemu ya 40 inatambua ndoa ya kiraia iliyofungwa katika nchi nyingine ikiwa ilifungwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo na wahusika walikuwa na uwezo wa kisheria wa kuoana chini ya Sheria ya Ndoa ya Kenya.
Sehemu ya 58 ya Sheria ya Ndoa ya Kenya inaruhusu Mkenya aliyefunga ndoa nje ya nchi kuomba ndoa hiyo isajiliwe na Msajili wa Ndoa nchini Kenya.
Sehemu ya 59 ya Sheria ya Ndoa inaeleza kuwa ndoa inaweza kuthibitishwa kwa kutumia cheti cha ndoa, nakala yake iliyothibitishwa au taarifa zilizomo kwenye sajili rasmi ya ndoa.
Hii ni muhimu hasa panapotokea migogoro ya kifamilia. Mjane anaweza kuhitaji kuthibitisha uhusiano wake na marehemu katika masuala ya mirathi. Vivyo hivyo, wanandoa wanapogawana mali baada ya kutengana, uthibitisho wa ndoa unaweza kuwa sehemu muhimu ya mchakato huo.
Kwa wale ambao hawajasajili ndoa zao, hatua ya kwanza ni kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Ndoa ili kufahamu utaratibu unaofaa kulingana na aina ya ndoa yao. Huduma za usajili zinapatikana pia kupitia tovuti ya eCitizen.
Ujumbe muhimu ni kwamba cheti cha ndoa si pambo la kuweka kwenye droo, bali ni stakabadhi muhimu ya kulinda haki za wanandoa. Ni bora kuhakikisha kila kitu kiko sawa wakati uhusiano unaendelea vizuri kuliko kusubiri msiba au mzozo ndipo mtu aanze kutafuta ushahidi wa ndoa yake.