Dimba

FIFA yaonya FKF dhidi ya kupeleka migogoro mahakamani

Na TOTO AREGE November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limeonya kuwa litachukua hatua dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayowasilisha migogoro inayohusiana na soka katika mahakama za kawaida nchini Kenya.

Katika barua iliyotumwa kwa kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Dennis Gicheru, FIFA ilisema imebaini ongezeko la kesi zinazohusu uongozi wa soka nchini zinazowasilishwa katika mahakama hizo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Afisa Mkuu wa FIFA anayesimamia vyama wanachama, Elkhan Mammadov, ilitumwa kwa FKF kupitia barua pepe Oktoba 5, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likipatiwa nakala.

FIFA ilisisitiza kuwa inalinda uhuru wa vyama vya soka kujiendesha na kupinga kupelekwa kwa migogoro ya soka katika mahakama za kawaida.

“Ukiukaji wowote wa kanuni hizi unaweza kuifanya FIFA kupeleka suala hilo kwa vyombo vyake husika ili kuzingatiwa kwa hatua zinazofaa kwa mujibu wa Katiba ya FIFA,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Shirikisho hilo liliitaka FKF kuhakikisha kuwa migogoro yote inayohusiana na soka nchini inatatuliwa kupitia njia rasmi zilizowekwa.

Liliashiria ibara ya 69 (1) ya Katiba ya FKF inayopiga marufuku kuwasilisha migogoro hiyo katika mahakama za kawaida. Vifungu vya pili na tatu vya ibara hiyo vinaelekeza kuwa migogoro hiyo isikilizwe kupitia mfumo wa usuluhishi.

FIFA ilisema migogoro hiyo inapaswa kuwasilishwa kwa chombo huru cha usuluhishi kinachotambuliwa na FKF au CAF, au Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) iliyoko Lausanne, Uswisi.

Kwa mujibu wa ibara ya 51 ya Katiba ya FIFA, wanachama hawaruhusiwi kupeleka migogoro katika mahakama za kawaida isipokuwa pale ambapo kanuni za FIFA au sheria zinazofunga kisheria zinaruhusu.

Nchini Kenya, Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Michezo (SDT) ndiyo yenye jukumu la kusikiliza kesi zinazohusiana na michezo.

Hata hivyo, baadhi ya wahusika ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya SDT wamekuwa wakikata rufaa katika Mahakama Kuu. Mwaka huu pekee, FKF imehusishwa katika angalau kesi tano katika mahakama hiyo.

Miongoni mwa kesi zilizovutia wengi ni ile ya kupandishwa na kushushwa daraja katika Ligi Kuu ya FKF, iliyowasilishwa na Kariobangi Sharks kupinga matumizi ya kanuni za 2025 ambazo zingesababisha timu hiyo kushushwa moja kwa moja hadi Ligi ya Taifa (NSL).

Pia, FKF iliwasilisha kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji ya Taifa (NEC) mwezi Aprili wa kumsimamisha rais Hussein Mohammed, Gicheru na mjumbe Yusuf Abdallah.

FIFA imeitaka FKF kuendelea kuijulisha kuhusu maendeleo muhimu katika kesi zinazoendelea mahakamani.