TAHARIRI: EACC ishirikiane na DCI kulinda pesa za wananchi
NA MHARIRI
SHERIA iliyoanzisha Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (CDF) mwaka wa 2003, ilikuwa na lengo la kuwawezesha wabunge kufadhili miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Seneta wa Nyandarua Bw Muriuki Karue alipochapisha Mswada wa kuilazimu Serikali ifadhili miradi katika maeneo bunge mwaka 1999, alikuwa na lengo tofauti.
Mswada huo ulipopitishwa na kuanza kutekelezwa miaka minne baadaye akiwa mbunge wa Ol-Kalou, ulitambua aina ya miradi inayofaa kufadhiliwa na Serikali Kuu.
Kifungu cha 22 cha sheria hiyo kinasema miradi itakayofadhiliwa na CDF yafaa kuwa (a) ya kunufaisha wakazi wote katika eneo (b) miradi ya michezo miongoni mwa mambo ya kuifaa jamii nzima.
Hata hivyo, sheria hiyo inaruhusu utumizi wa pesa za CDF kununua magari, mashine na vifaa vingine, mradi tu viwe vya kutumiwa na eneobunge.
Ufichuzi kuwa basi lililonunuliwa kwa Shule ya Upili ya St Steven’s jijini Nairobi sasa limegeuzwa mali ya mtu binafsi na linatumika katika uchukuzi wa umma unakera.
Basi hilo lilinunuliwa kwa fedha za Hazina ya Eneobunge la Embakasi Kusini mwaka wa kifedha wa 2014/15.
Kwamba basi hilo limekuwa likitumika kwa uchukuzi wa umma chini ya kampuni ya City Shuttle, ni kuonyesha limekuwa mali ya mtu binafsi anayejikusanyia maelfu ya pesa kila siku, ilhali lilinunuliwa kutumia pesa za mwananchi.
Ufichuzi huu huenda ni asilimia ndogo mno ya visa vingine ambapo maafisa waliopewa afisi za umma wanatumia pesa ya mwananchi katika miradi ya kibinafsi.
Huu ni utumizi mbaya wa mamlaka ambao kisheria, anayehusika anapaswa kuwa amerekodi taarifa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Tabia hii ya watumishi wa wananchi kugeuka na kutumia pesa na raslimali za umma kujinufaisha imekithiri sana, hasa miongoni mwa wanasiasa. Katika baadhi ya maeneo bunge, wanakamati wa CDF ni wapenzi wa pembeni, familia, marafiki au maajenti wa kampeni wa wabunge.
Pesa zozote zinazotokana na jasho la mwananchi zafaa kulindwa dhidi ya watu wanaojinufaisha. Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI), Bw George Kinoti, anapaswa kuanzisha uchunguzi wa kisa hiki cha Embakasi Kusini. Asikome hapo. Watu wengine wote wanaonifausha na pesa za mwananchi yafaa waandikishe taarifa na kisha wafunglliwe mashtaka kortini.