Habari za Kitaifa

Afrika itapiga hatua tu iwapo vijana watakwezwa, Mvurya ashauri

Na CECIL ODONGO June 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Kenya imesema kuwa itaendelea na mipango yake ya kuwekeza kwenye miradi ya kuwainua vijana na kushirikiana nao katika uvumbizi wa teknolojia.

Waziri wa Masuala ya Vijana na Uchumi Bunifu Salim Mvurya amesema kuwa Kenya na mataifa mengine Afrika, yanastahili  kumakinikia utekelezaji wa  miradi ya kuwainua vijana badala yao  viongozi kuwatumia tu kuendeleza maslahi yao kisiasa.

Bw Mvurya alisema kuwa vijana watastahiwa na kuenziwa kupitia ufanisi wao kwenye nyanja za kibiashara , mipango inayotoa nafasi za kazi na utatuzi wa changamoto za kijamii.

“Vijana wa Afrika wamezungumza na wanataka kazi na si mapeni machache, wanataka uwajibikaji na si ahadi na huu ndio ukweli. Vijana hawana subira bali wana nia ya kuafikia ndoto zao,” akasema Bw Mvurya.

Alikuwa akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la CorpsAfrica 2025 ambalo liliwashirikisha zaidi ya vijana 1,000 kutoka mataifa 11 Afrika. Kongamano hilo liliandaliwa katika Chuo cha Serikali (KSG).

Vijana walioshiriki kongamano, ambao wengi wao wamekuwa wakishiriki kazi za kujitolea walitoka, Kenya, Malawi, Ghana, Rwanda, Morocco, Senegal, Ethiopia, Uganda, Gambia, Afrika Kusini na Côte d’Ivoire.

Afisa Mkuu Mtendaji  na mwanzilishi wa CorpsAfrica Liz Fanning, alisema kuwa ana uhakika kuna suluhu kutokana na changamoto zinazowaandama vijana Afrika.

Bi Fanning alisema malengo ya CorpsAfrica ni kuwakuza vijana ili wawe viongozi bora wa Afrika ambao watatumikia jamii na kuchangia ukuuaji kutoka nyanjani.

“Kuna nafasi na sauti za vijana inaweza kusikizwa na washirikishwe katika kuamua masuala muhimu ya Afrika,” akasema Bi Fanning.

Dkt Kingóri Mugendi ambaye amekuwa mstari wa mbele kupambania maslahi ya vijana, alisema ajira katika nyanja mbalimbali ndiyo itawezesha vijana kujikimu na kumakinikia uvumbuzi.