Serikali ilivyozima mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege
MAMIA ya wasafiri wa kimataifa na wa humu nchini walikwama baada ya wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kugoma.
Walikuwa wanalalamikia mpango tata wa serikali kukodisha uwanja huo kwa kampuni ya Adani Group kutoka India.
Serikali ililazimika kuchukua hatua za haraka kuzungumza na viongozi wa wafanyakazi hao wakarejea kazini baada kulemaza shughuli kwa zaidi ya saa 16.
Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir na Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi Kenya (Cotu) Francis Atwoli waliongoza mazungumzo ya kumaliza mgomo huku wakisisitiza kuwa kutakuwa na uwazi katika mpango wa kukodisha uwanja huo ikiwa ni pamoja na kushirikisha wafanyakazi.
Mgomo huo ulifutwa baada ya hasara kubwa kukadiriwa huku wafanyakazi wa viwanja vingine vikuu vya ndege katika majiji ya Mombasa, Kisumu na Eldoret wakigomba kuunga wenzao wa JKIA.
Kampuni za Safari za Ndege ziliarifu wateja kwamba mgomo huo uliathiri shughuli katika uwanja huo na kufanya safari kucheleweshwa au kufutwa.
Mgomo huo ulisababisha maelfu ya abiria kukwama katika kanda ya Afrika Mashariki huku mashirika ya usafiri na uchukuzi wa ndege yakisitisha safari kupitia Kenya.
Kampuni za ndege za Rwandair, Ethiopian Airlines na Ugandan Airlines zilishauri wateja wao kusubiri kwa kuwa shughuli katika JKIA zilikuwa zimelemazwa.
Chama cha wafanyikazi wa viwanja vya ndege kilitangaza mgomo huo kuanzia saa sita usiku Jumatano baada ya kubainika kuwa serikali ya Kenya inalenga kukodisha JKIA kwa kampuni ya Adani Group ya India kwa miaka 30, huku kikihofia hatua hiyo itasababisha wanachama kupoteza kazi.
Mnamo Jumanne, Mahakama Kuu ya Kenya iliahirisha kwa muda mipango iliyopendekezwa ya kukodisha uwanja huo wa ndege hadi Oktoba 8 kusubiri kesi iliyowasilishwa na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya na Chama cha Wanasheria cha Kenya kuamuliwa.
Katika taarifa Jumatano wasimamizi wa JKIA na shirika la ndege la Kenya waliomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na mgomo huo.
“Kenya Airways ingetaka kuarifu kwamba kutokana na mgomo wa baadhi ya wafanyakazi katika JKIA, kumekuwa na ucheleweshaji wa safari za kuondoka nchini na kuwasili kwa abiria,” Kenya Airways ilisema kwenye taarifa Jumatano.
Kampuni ya Jambojet, inayotoa huduma za uchukuzi wa ndege ndani ya nchi, pia ilitoa taarifa kama hiyo.
Wakitangaza mgomo, viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya Kenya (Kawu) walisema serikali haikuonyesha nia njema katika mfululizo wa mazungumzo kuhusu mpango wa kukodisha uwanja huo.
“Serikali haijakuwa na uwazi na nia njema. Hawajatupa stakabadhi zote tulizodai. Tunachotaka ni serikali ikomeshe mpango wa kukodisha uwanja kwa Adani,” Katibu Mkuu wa Kawu, Bw Moss Ndiema aliambia Taifa Leo.
Serikali ilisema kwamba katika mpango huo, kampuni hiyo ya India itaboresha uwanja wa ndege, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya pili ya ndege na kituo kipya cha abiria chini ya mkataba wa miaka 30 wa kujenga- kuendesha na hatimaye kuhamisha kwa serikali.
Wafanyakazi hao walitishia kugoma wiki moja iliyopita lakini baadaye walisitisha mgomo huo baada ya kuzungumza na serikali katika mkutano uliofanyika Ikulu.
Miongoni mwa masuala muhimu waliyoibua ni pamoja na kuwepo kwa watu wasiowafahamu, wanaodaiwa kuwa wafanyikazi wa Adani ambao wamekuwa wakizunguka JKIA wakishirikiana na maafisa wakuu wa usalama wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege ya Kenya.
Ili kusitisha mgomo, wafanyakazi hao walitaka “shughuli za siri, zisizojulikana na zisizoelezeka za wafanyakazi wa Adani na maajenti wake kusitishwa na kukomeshwa mara moja.”
Pia walitaka ufichuzi kamili wa maelezo ya pendekezo la kukodisha uwanja wa ndege kwa Adani na wakabidhiwe stakabadhi hizo ili wazichunguzwe kabla ya kitu kingine chochote kutendeka.
Stakabadhi hizi, walisema, zitawafahamisha mchango wao wa maana katika awamu ya ushirikishi wa umma wa mradi.
Jumatatu, Bw Atwoli alisema stakabadhi hizo zilitolewa na watazikagua kwa siku 10 kabla ya kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo huku Bw Ndiema akisema hawakukubali mpango wa kukodisha uwanja kwa Adani.
“ Nataka kusema hivi: hatujakubali Adani,” alisema.
Bw Chirchir alikiri kuwa serikali ilifeli katika mawasiliano yake kuhusu mpango huo.
Wafanyikazi hao pia walitaka kusimamishwa kwa safari iliyokusudiwa ya ujumbe wa watu 16 kwenda India katika lengo la kuendeleza ukodishaji wa uwanja wa ndege kwa Adani hadi zoezi la ushiriki wa wadau na umma litakapokamilika na “Wakenya wakubali mradi huo.”
Mgomo huo ulitatiza kwa kiasi kikubwa biashara za sekta ya kibinafsi zinazotegemea sekta ya usafiri wa angani, zilizopata hasara ya mamilioni ya pesa.
Chama cha Wasafirishaji wa Mazao kama maua, matunda na mboga kilikadiria kuwa wanachama wake watapoteza takriban Sh410 milioni kila siku ya mgomo huo
“Sekta hii inauza nje kati ya tani 600 na 800 za mazao kila siku kupitia ndege za mizigo na abiria na ikiwa wafanyakazi wa KAA hawafanyi kazi hatuwezi kusafirisha mizigo. Huu ni usumbufu mkubwa unaoathiri biashara yetu,” Afisa Mkuu Mtendaji wa FPEAK Hosea Machuki aliambia Taifa Leo.
Sekta ya usafiri pia ilipata hasara ya mamilioni kutokana na mgomo huo, huku Muungano wa Maajenti wa Usafiri Kenya (Kata) ukikadiria kuwa siku moja ya mgomo huo iliwagharimu angalau Sh2.06 milioni mauzo ya tikiti pekee.
RIPOTI ZA NDUBI MOTURI, STEVE OTIENO, VINCENT OWINO NA JULIUS BARIGABA