Kimataifa

Kagame azoa asilimia 99 ya kura za urais Rwanda

Na MASHIRIKA July 16th, 2024 2 min read

KIGALI, RWANDA

RAIS Paul Kagame wa Rwanda ameshinda urais tena kwa muhula wa nne mfululizo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Rwanda mnamo Jumatatu.

Wapigakura waliosajiliwa mwaka huu walikuwa milioni tisa huku katika kura milioni saba zilizokuwa zimehesabiwa, Rais Paul Kagame akipata asilimia 99.15.

Frank Habineza wa chama cha Green Party of Rwanda (DGPR) alipata asilimia 0.53 ya kura zilizohesabiwa huku mgombeaji huru, Phillipe Mpayimana akipata asilimia 0.32.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi, Bi Oda Gasinzigwa alisema kwamba shughuli ya kuhesabu kura linaendelea.

Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Rais Paul Kagame aliwapongeza wananchi wote walioshiriki shughuli ya uchaguzi.

Aliwapongeza pia kwa namna ya kipekee wakuu wa vyama mseto vya siasa vilivyoungana na chama tawala cha RPF.

“Matokeo haya ni kutokana na kuungana kwa wanachama wetu wa RPF na wafuasi wa vyama vingine walioshirikiana nasi,’’ alisema Kagame akiwanyooshea mkono wa shukrani viongozi hao waliokuwa wamesimama nyuma yake.

Kiongozi wa chama cha Green Party cha Rwanda, Frank Habineza mara baada ya kutolewa matokeo alimpongeza Rais Kagame kwa ushindi huo huku Pillipe Mpayimana akisema hata kama hesabu zinaonyesha ameshindwa, bado ana imani kwamba atafanya vizuri siku za usoni
Alisema kikubwa kwake ni kwamba alionyesha uzalendo wake kwa kugombea kiti cha urais.

Zaidi ya watu milioni tisa walisajiliwa kama wapiga kura huku milioni mbili kati yao wakipiga kura kwa mara yao ya kwanza wengi wao wakiwa ni vijana wa chini ya miaka 20.

Matokeo haya yanakamilisha mchakato wa kupiga kura na kampeini za uchaguzi ambapo ilitarajiwa kuwa Kagame ambaye ameiongoza Rwanda kwa miaka 24 ataibuka mshindi na kuwa uongozini kwa muhula wa nne mfululizo.

Kagame ambaye ni mwanajeshi kitaaluma wakati wa kampeni zake alisema mara kadhaa kwamba angeshinda uchaguzi huo kutokana na mchango wake katika maendeleo ya Rwanda.

Kadhalika, alisema kwamba alikubali kugombea ili kukidhi mahitaji ya raia waliomuomba siku zote kugombea urais tena.

Mara baada ya kukamilisha kampeni za uchaguzi alisema kwamba anaendelea kuwaomba wanachama wa chama chake kuendelea kufikiria mtu atakayechukua nafasi yake hapo baadaye kwani kwa maoni yake wakati umefika mtu mwingine achukue hatamu za uongozi.