Maoni

MAONI: Wakenya wasitishwe na yeyote, waendelee kuangazia mapungufu ya serikali

Na KINYUA KING’ORI December 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MATAMSHI yanayotolewa na baadhi ya viongozi, wakiwemo mawaziri ni ya kukera na kuudhi huku Wakenya wakionekana kuendelea kukosa imani na namna serikali ya Kenya Kwanza inavyoshughulikia mipango ya maendeleo.

Je, ni kipi kilibadilika kwa viongozi waliochaguliwa kushindwa kuibuka na sera bora na maoni faafu kuimarisha uchumi na maendeleo ya taifa?

Je, kwa nini maafisa wakuu serikalini watishie raia wanaokosoa serikali kwa kutekeleza sera kandamizi na miradi muhimu bila kuzingatia maoni yao?

Kukosoa au kusifia serikali ni wajibu wa raia wanaotawaliwa. Ni haki yao ya kikatiba ambayo haiwezi kuondolewa na vitisho vya Rais William Ruto au mawaziri wake.

Viongozi wanaweza kufurahisha raia kwa kujitolea kikamilifu kutimiza ahadi zao na kurekebisha kasoro zinazokosolewa kuimarisha imani kwao na kushangilia ubora katika kutekeleza majukumu yao.

Inatamausha kuona hata viongozi waliokuwa wakikosoa serikali usiku na mchana kwa kufeli kuwajibikia wananchi, wamegeuka watetezi sugu wa serikali ile ile.

Ikiwa viongozi wameshirikiana kuunda serikali jumuishi kulinda manufaa yao, wananchi hawana budi kushirikiana pia bila kuzingatia ukabila kukabiliana na maafisa serikalini wanaokwamiza ustawi.

Jiulize kama si Wakenya kujitokeza kupinga ujenzi wa uwanja wa JKIA uliogubiikwa na wingu la ufisadi ingekuwaje iwapo dili ya ujenzi huo ingeendelea?

Umoja wa siafu humtorosha nyoka kwenye shimo, hivyo Rais Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na hata Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wakiungana kwa manufaa yao, raia wafaa washirikiane kuhakikisha wanatumia nguvu na muda katika mitandao ya kijamii na hafla mbalimbali vijijini kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupinga sera potovu, miradi yenye ufisadi, ukiukaji wa katiba na vitisho vinavyoendeshwa serikalini.

Ni ukosefu wa shukrani kwa kiongozi kukerwa na wananchi wanaoelezea hisia zao kuhusu maovu yanayotatiza utekelezaji wa maendeleo.