Wanyama kupata timu yaibua madai huenda akarudi Harambee Stars
HATUA ya nahodha wa zamani wa timu ya taifa Harambee Stars, Victor Wanyama, kujiunga na klabu ya Dunfermline Athletic ya Scotland, kumeibua madai kuwa siku zijazo huenda akaghairi nia na kurejea kusakatia timu ya taifa.
Wanyama alijiunga na klabu hiyo inayonolewa kocha wa zamani wa Celtic Neil Lennon, kama mchezaji huru. Dili yake itadumu hadi mwishoni mwa msimu.
Dunfermline Athletic inashiriki Ligi ya Daraja la Pili la Scotland na kwa sasa ipo ya pili kutoka mkiani kati ya timu 10. Ujio wa Wanyama unatarajia kuipiga jeki timu hiyo inapopambana kusalia ligini.
Wanyama awali alisema alipokea ofa lakini si wengi walitarajia kuwa angejiunga na timu inayoshiriki daraja la pili Scotland.
“DAFC ina furaha kutangaza kuwa imemsajili mwanadimba wa kimataifa wa Kenya Victor Wanyama kwa mkataba ambao utadumu hadi mwishoni mwa msimu,” ikasema taarifa ya DAFC.
Wanyama hajakuwa na timu tangu aagane na Montreal FC ya Canada mnamo Novemba mwaka jana.
Anakumbukwa kwa kufungia Celtic katika ushindi wa 2-1 dhidi ya miamba Barcelona kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla kuelekea Southampton mwaka 2013.
Alijiunga na Tottenham Hotspur akihamia huko na kocha wake Mauricio Pochettino. Alisakatia Spurs kwa miaka mitano kisha akajiunga na Montreal CF ambapo alisakata mechi 117 na kufunga mara tano.
Hata hivyo, wengi wa mashabiki mitandaoni wanaona hatua ya Wanyama kujiunga na Dunfermline Athletic ni dalili kuwa huenda ananoa makali yake ili arejelee kuchezea Stars.
“Wanyama si mzee na akijitahidi na kuwa kwenye fomu nzuri, milango ya timu ya taifa haijafungwa. Ni mapema kusema atafuatiliwa kwa sababu lazima fomu yake ionekane,” akasema mmoja wa watu wenye ushawishi Stars ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.
Wanyama alitangaza kustaafu Harambee Stars mnamo Septemba 27, 2021 akiwa na umri wa miaka 30. Mara ya mwisho alichezea Stars ni Novemba 15, 2020 dhidi ya Comoros kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Afrika 2022.
Ilidaiwa alikasirishwa na hatua ya kocha wa wakati huo Jacob ‘Ghost’ Mulee kumpokonya unahodha na kumpa mshambulizi wa Al Duhail Michael Olunga.
Hii ilikuwa baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Uganda kwenye mechi ya ufunguzi ya kufuzu Kombe la Dunia 2022. Alichezea Harambee Stars mechi 60 baada ya kucheza mara ya kwanza 2007 na alipewa unahodha 2013 kutoka kwa Dennis Oliech.
Anakumbukwa kwa kuongoza Kenya kwenye mechi za ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2019.