Bambika

Nuru Okanga adhihirisha ni wembe masomoni

February 17th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MFUASI na mtetezi sugu wa kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, Nuru Okanga, kwa mara nyingine amedhihirisha ni wembe masomoni baada ya kutoa ufafanuzi sahihi wa maana ya Biolojia.

Okanga aliyefanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka 2023 alifichulia wafuasi wake kupitia chapisho kwa ukurasa wake wa Facebook akisema kwamba baada ya kuhudhuria somo la Biolojia, sasa ameanza kushikanisha maana ya baadhi ya dhana na maneno ya kitaaluma.

Okanga alieleza kwamba tofauti na awali ambapo alikuwa akisikia tu kutoka kwa waliomtangulia kukanyaga guu katika Kidato cha Kwanza, sasa ni yeye mwenyewe anayejua maana ya dhana muhimu kuhusu somo hilo ambalo ni la sayansi.

Hata hivyo alisifia somo hilo, ambalo alisema si ngumu kwani aligundua ni kuhusu maisha.

“Ufafanuzi rahisi wa bayolojia. Bio humaanisha maisha na -olojia humaanisha kusoma. Kwa hivyo, biolojia humaanisha elimu kuhusu uhai. Biolojia ni somo la viumbe vilivyo hai (na viumbe vilivyokufa, kama vile visukuku). Biolojia huweka zingatio kwa jinsi viumbe hivi vinavyokuja kuwa, namna vinavyojiendeleza na kutagusana katika mazingira yao halisi,” akaeleza Okanga.

Okanga ambaye anapenda siasa sana, ni mtu wa familia.

Alisema hakuna kulaza damu shuleni isipokuwa kujifunza kwa kuwasilikiza walimu wake wanapofundisha.

Ana azma ya kuwania nafasi ya uwakilishi wadi Kholera katika uchaguzi mkuu wa 2027.