Habari za Kitaifa

Polisi wa Kenya wapata ushindi wa kwanza Haiti kwa kukomboa bandari kutoka kwa magenge


MAAFISA wa polisi wa Kenya nchini Haiti na wenzao wa Haiti wamefanikiwa kukomboa bandari ambayo imekuwa ikidhibitiwa na magenge kwa muda wa miezi mitano iliyopita.

Maafisa hao, ambao ni sehemu ya kikosi cha kudumisha usalama cha kimataifa (MSS), Jumatano walifanikiwa, kutwaa tena bandari ya Auorite Portuaire Nationale (APN), ambayo ilitekwa na magenge mnamo Machi 6, 2024.

Bandari hiyo iko katika Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti.

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Alhamisi, Julai 18, Kamanda wa MSS Godfrey Otunge alisema magenge hayo yalisalimisha bandari baada ya ufyatulianaji wa risasi.

“Kikosi cha Kenya na maafisa wa polisi wa Haiti walifanikiwa kufukuza magenge yaliyokuwa yameanza kuwafyatulia risasi. Maafisa hao kisha walitwa bandari iliyokuwa ikidhibitiwa na magenge hayo,” alisema Bw Otunge.

Kwa kutwaa bandari, magenge hayo yalizuia chakula, matibabu na vifaa vingine, ikiwa ni pamoja na misaada ya kibinadamu, kuingia katika taifa hilo la Caribbean.

Bandari hiyo ilikuwa mojawapo ya sehemu zilizosalia za kuingia Haiti zinazotumiwa na Umoja wa Mataifa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wananchi, ambao wengi wao hawana uwezo wa kujikimu.

Makabiliano kati ya maafisa hao na magenge hayo yalifanyika mita chache tu kutoka Ikulu ya White Palace, makazi rasmi ya rais wa Haiti.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa maafisa wa Kenya kuwahusisha wanachama wa genge katika vita walipokuwa wakisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture hadi bandari ya Autorite Portuaire Nationale.

Bw Otunge alisema operesheni ya Jumatano ilikuwa ya kwanza kufanyika katikati mwa jiji.

“Maafisa wa Kenya na Haiti walikuwa chonjo katika maeneo kadhaa jijini huku ufyatulianaji risasi ukiendelea na kufanikiwa kuingia bandarini, ambayo haingefikika tangu Machi,” alisema.

Hapo awali, polisi wa Kenya nchini Haiti waliombwa kulinda miundombinu muhimu na kushika doria mitaani huku wakijifunza polepole kuhusu operesheni za magenge hayo.

Kuingia kwao bandarini na kufukuza wanachama wa genge hilo kulikuja saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille kutangaza hali ya hatari katika manispaa 14 zinazodhibitiwa na genge.

“Ninaidhinisha Polisi wa Kitaifa wa Haiti, kwa msaada wa Vikosi vya Wanajeshi vya Haiti na MSS, kuanzisha operesheni katika maeneo yaliyoathiriwa,” Bw Conille alisema.