Michezo

UEFA: Arsenal ndani ya 16-bora, Man City hesabu ni ngumu

Na GEOFFREY ANENE, MASHIRIKA January 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA:

WANABUNDUKI wa Arsenal walipiga hatua kubwa ya kuingia 16-bora moja kwa moja kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuchabanga Dinamo Zagreb 3-0 uwanjani Emirates Jumatano, katika siku ambayo Manchester City walipepetwa 4-2 na Paris St Germain (PSG) na kujiweka hatarini kubanduliwa mapema.

Vijana wa kocha Mikel Arteta walidumisha rekodi yao nzuri ugani Emirates kwenye UEFA hadi mechi nane tangu msimu jana na pia kutofungwa bao katika idadi sawa ya michuano kwenye shindano hilo.

Arsenal walinyamazisha vijana wa Fabio Cannavaro mabao kupitia kwa Declan Rice (lake la kwanza kabisa kwenye Klabu Bingwa), Kai Havertz na Martin Odegaard. Goli la Rice lilipatikana sekunde ya 104. Ni la mapema kabisa Arsenal imepata tangu Yaya Sanogo (sekunde 72 mwezi Novemba 2014).

Martin Odegaard (kushoto) wa Arsenal atumbukiza goli wavuni kumpita kipa Ivan Nevistic wa Dinamo Zagreb, mechi hiyo ya UEFA. PICHA | REUTERS

“Mwezi huu ni muhimu sana. Ni wakati mgumu kwa sababu tuna mechi tisa. Tunafurahia kupata ushindi leo, lakini sasa tunaelekea Wolves kwa majukumu ya ligi na tunajua si kibarua rahisi,” akasema Arteta.

Mhispania huyo alikaribisha kikosini mvamizi Ethan Nwaneri kutoka mkekani baada ya mechi nne na kuonjesha mshambulizi Nathan Butler-Oyedeji,22, mechi ya watu wazima kwa mara ya kwanza.

Ushindi umepaisha Arsenal kutoka nafasi ya nane hadi tatu. Wana alama 16, pazuri zaidi kufuzu 16-bora moja kwa moja kwa kumaliza ndani ya nane-bora.

Mabingwa watetezi Real Madrid nao walifufua matumaini ya kusalia mashindanoni baada ya kunyeshea Salzburg 5-1 kupitia mabao ya Rodrygo na Vinicius Junior (mawili kila mmoja) na Kylian Mbappe. Mads Bidstrup alipachika bao la Salzburg kujifariji.

Vinicius sasa ni Mbrazil wa pili tu nyuma ya Ronaldo Nazario kufungia Real zaidi ya mabao 100. Mshindi huyo wa tuzo ya mwanasoka bora dunia wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) sasa amefungia Real jumla ya mabao 101 katika mashindano yote, matatu nyuma ya jagina Nazario.

Hata hivyo, mambo yalikuwa telezi kwa Man City jijini Paris, Ufaransa, wakitupa uongozi wa mabao 2-0 kuishia katika kichapo chungu mikononi mwa PSG.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola (kulia), na fowadi Jack Grealish washangaa timu hiyo kutupa uongozi dhidi ya PSG mechi yao ya UEFA, Jumatano. PICHA | REUTERS

PSG walitoka chini mabao mawili kwa mara ya kwanza katika historia ya UEFA kuduwaza wageni wao hao 4-2 kupitia mabao ya Ousmane Dembele (dakika ya 56), Bradley Barcola (60), Joao Neves (78) na Goncalo Ramos (90+3).

Vijana wa kocha Pep Guardiola waliongoza 2-0 baada ya kufunga mabao mawili ya haraka mwanzo wa kipindi cha pili kutoka kwa Jack Grealish (50) na Erling Haaland (53), lakini wakapatia PSG matumaini wakati Dembele alikomboa goli moja kutokana na asisti ya Barcola. Kutoka hapo, City walikuwa taabani hadi kipenga cha mwisho.

Ulikuwa pia usiku wa giza nene kwa washindi wa zamani Bayern Munich walioangushiwa kichapo chungu cha 3-0 kutoka kwa wenyeji Feyenoord.

Bayern walichezesha nyota wao wote wakali wakiwemo Jamal Musiala, Michael Olise na Harry Kane na kusukuma makombora 30 dhidi ya nane tu, lakini wakaduwazwa na mabao kutoka kwa Santiago Gimenez (mawili ikiwemo penalti) na Ayase Ueda.

Kocha Vincent Kompany amelaumu kikosi chake chote cha Bayern kwa kutolinda ngome yao vyema. Hata hivyo, aliongeza kuwa hawaogopi kutumbukia katika mduara wa tisa hadi 24 ambapo timu lazima zitashiriki mchujo ili kuwania tiketi ya kuingia 16-bora.

Leipzig nao walimaliza msururu wa vipigo sita mfululizo kwa kunyuka Sporting 1-0 nchini Ujerumani. Benjamin Sesko na Yussuf Poulsen walifunga mabao ya Leipzig naye Viktor Gyokeres akapata la Sporting kufutia machozi.

MATOKEO YA UEFA (JUMATANO):

Leipzig 2-1 Sporting

Shakhtar Donetsk 2-0 Brest

Sparta Prague 0-1 Inter Milan

Feyenoord 3-0 Bayern Munich

Arsenal 3-0 Dinamo Zagreb

AC Milan 1-0 Girona

PSG 4-2 Manchester City

Real Madrid 5-1 Salzburg

Celtic 1-0 Young Boys