Siasa

Ruto, Kindiki kuvamia ngome ya Gachagua kwa kishindo

Na GITONGA MARETE March 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto sasa yuko tayari kuwakabili wakazi wa Mlima Kenya uso kwa macho atakapoanza ziara yake eneo hilo ambalo kwa sasa linaonekana kudhibitiwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mara ya mwisho Rais alipokuwa Mlima Kenya ni Novemba 16 alipohudhuria sherehe ya kumtawaza Askofu wa Katoliki Jimbo la Embu Peter Kimani Ndung’u.

Kufika leo, Rais Ruto hajakanyaga Mlima Kenya kwa siku 121 huku akiwa ametalii Nyanza, Magharibi, Bonde la Ufa, Kaskazini Mashariki, Pwani na Nairobi na kuzindua miradi ya maendeleo.

Mbali na Mlima Kenya, Rais pia amekawia sana kuzuru eneo la Ukambani, ngome ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye amekuwa mstari wa mbele kukosoa utawala wake.

Ziara hiyo inayotarajiwa hivi karibuni itakuwa ya kwanza ya kisiasa kwa Rais tangu Bw Gachagua abanduliwe katika unaibu rais mnamo Oktoba mwaka jana.

Mlima Kenya (Nakuru ikiwemo) ilikuwa ngome ya kisiasa ya Rais mnamo 2022 ambapo alizoa jumla ya kura milioni 2.8 kati ya milioni 7.2 alizopata na kuwahi ushindi dhidi ya Raila Odinga wa Azimio la Umoja.

Duru zinasema kuwa Rais Ruto ataanza ziara yake Mlima Kenya Mashariki ambako Naibu Rais Prof Kindiki anatoka kabla ya kuelekea Mlima Kenya Magharibi ambako Bw Gachagua ana ushawishi na usemi mkubwa kisiasa.

Katika kujitayarisha kwa ziara hiyo, Prof Kindiki aliandaa mkutano na wabunge 54 kutoka eneo hilo Alhamisi wiki hii ambapo inadokezwa aliwaambia wamlaki Rais kwa dhati na heshima zote.

Wabunge hao walitoka katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nakuru, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Embu, Meru na Tharaka-Nithi.
Katika kikao hicho Prof Kindiki na wabunge hao walizungumza kuhusu miradi ya maendeleo iliyoanzishwa, mahali ambapo imefikia na ile itakayozinduliwa.

Mnamo Machi 6, Prof Kindiki alikutana na wabunge kutoka maeneo yanayokuza kahawa ambapo walizungumizia changamoto na ufanisi wa sekta hiyo iliyokuwa ikithaminiwa sana na Bw Gachagua.

Aidha, Prof Kindiki amekuwa akikutana na madiwani na wanasiasa kutoka Mlima Kenya, suala kuu likiwa miradi ya ustawi.
Kwenye baadhi ya mikutano hiyo, amemchemkia Bw Gachagua kwa “kuendeleza siasa za kuwachochea raia dhidi ya serikali”.

Mbali na kahawa, miradi inayotarajiwa kuzinduliwa ni barabara za Mau Mau, Kenol-Marwa, mabwawa, masoko na miradi mingine ya kilimo.

“Kwa naibu rais tulithamini ziara ya rais na miradi inayolenga kufufua sekta ya kilimo cha kahawa, chai, viazi, miraa, makademia, muguka na mpunga. Pia tuliangazia ufugaji wa mifugo na kuku,” akasema mbunge mmoja aliyehudhuria mkutano huo ambaye aliomba asitajwe jina.

Mbunge wa Imenti ya Kati, Kirima Ngucine alithibitisha kuwa Rais atatua Mlima Kenya hivi karibuni kuzindua miradi mbalimbali na akakanusha kuwa eneo hilo limetengwa katika utawala wa sasa.

“Ndiyo, tunajiandaa kwa ziara ya Rais lakini hatujaambiwa tarahe kamili ya ujio wake na ratiba yenyewe. Atazindua miradi iliyokwama ambayo imetengewa pesa za kuimaliza,” akasema Bw Ngucine kupitia mahojiano ya simu.

Mbunge mwengine kutoka Meru alisema Rais anatarajiwa Mlima Kenya wiki tatu zijazo lakini bado hawajakubaliana kuhusu miradi ambayo ujenzi wayo utazinduliwa.

Mnamo Februari 28 akiwa nyumbani kwake Irunduni, Tharaka-Nithi, Prof Kindiki aliwaomba wakazi wa Mlimani wamkaribishe Rais akizuru eneo hilo.

“Akija Rais huku naomba apewe makaribisho ya heshima kwa sababu tunataka kusonga mbele pamoja bila kumwacha yeyote nyuma,” akasema alipokuwa mwenyeji wa viongozi wa mashinani Embu, Tharaka-Nithi, Meru na Isiolo.

“Si vyema kwa wachochezi waendelee kuwadanganya Wakenya kwa sababu barabara nyingi za hapa zilikwama 2018. Wakati huo hakuna aliyewachochea watu dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ilhali sasa wanataka Rais Ruto ndio alaumiwe,” akasema Profesa Kindiki.

Naibu Rais amekuwa akikwepa siasa za ubabe dhidi ya Bw Gachagua mlimani lakini amewahi kumkashifu mtangulizi wake kuwa Rais Ruto atahudumu kwa muhula moja pekee.