Mivutano yaibuka upya katika upinzani
UPINZANI nchini unakabiliwa na mivutano mipya ya ndani baada ya Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua kupendekeza muungano wa vyama vitatu, hatua iliyozua malumbano na viongozi wengine wanaolenga kumwondoa Rais William Ruto mamlakani 2027.
Bw Gachagua anataka DCP, Linda Mwananchi ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka ziungane.
Katika mahojiano na runinga ya Inooro, Bw Gachagua alisema muungano wa Mlima Kenya, Magharibi na Ukambani unatosha kuushinda utawala wa Rais Ruto.
Alidai ana uwezo wa kuleta kura milioni 10, huku Bw Sifuna akileta milioni nne na Bw Musyoka milioni tatu.
“Baina yangu, Sifuna, Eugene Wamalwa na Kalonzo Musyoka, uchaguzi utakuwa umekwisha. Hata tusipopata wengine, bado tunaweza kushinda,” akasema Bw Gachagua.
Hata hivyo, pendekezo hilo limewakera baadhi ya viongozi wa upinzani, wakiwemo kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang’i na Kiongozi wa DP Justin Muturi, ambao wamemshutumu Bw Gachagua kwa kiburi na kuwadharau washirika wake.
Dkt Matiang’i alisema matamshi ya Bw Gachagua yanahatarisha kuuvunja upinzani kwa kuugawanya kwa misingi ya kikabila.
“ Kiburi cha walio wengi na majivuno hayo ndiyo yatakayougawanya upinzani na kufanya iwe vigumu kuungana,” akasema
Aliongeza kuwa uongozi wa nchi haupaswi kuamuliwa kwa misingi ya jamii, bali uwezo wa mtu binafsi.
Bw Muturi naye alisema kwamba hakuna jamii moja inayoweza kumwezesha mtu kuwa Rais bila kuungwa mkono na Wakenya kutoka maeneo mengine.
“Urais hupatikana kupitia maafikiano ya kitaifa, miungano ya kimkakati na uwezo wa kuwaunganisha Wakenya kutoka jamii na maeneo mbalimbali,” alisema.
Alionya kuwa mpango wa vyama vitatu si njia ya moja kwa moja ya kuingia Ikulu na akataka muungano ujengwe kwa kuheshimiana, badala ya vitisho na mashindano ya ubabe.
Mivutano hiyo inatokana pia na madai ya baadhi ya viongozi kuwa washirika wao ni vibaraka wa serikali. DCP imehusisha madai hayo na Bw Matiang’i na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wa People’s Party of Kenya.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa mzozo huo unahusu pia udhibiti wa kura za eneo la Mlima Kenya.
Aidha, viongozi hao hawajakubaliana kuhusu atakayekuwa mgombea mmoja wa urais wa upinzani. Wengi wana matarajio ya kuwania kiti hicho, huku maswali yakiibuka kuhusu uwezo wao wa kuvutia uungwaji mkono wa kitaifa, fedha na miundo ya kisiasa.
Dkt Matiang’i alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea mwingine iwapo atachaguliwa kupitia mchakato wa wazi na unaowashirikisha wote.
“Yeyote atakayechaguliwa kupitia mchakato jumuishi na unaokubalika kwetu sote, nitamuunga mkono,” akasema.
Alisema pia kuwa akichaguliwa Rais, atafuta ushuru wa nyumba, kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama na kuhakikisha rasilimali za kaunti zinatumika ipasavyo.