• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Wakazi wakejeli maafisa kushindwa kuwakamata wahalifu

Wakazi wakejeli maafisa kushindwa kuwakamata wahalifu

Ahmed Omar akilalamika juu ya idadi kubwa ya wahalifu wanaozidi kuwakosesha amani wakazi kisiwani Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kisiwa cha Lamu wameilalamikia idara ya usalama eneo hilo kwa kutowakamata wahalifu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi hao kwa kupora simu zao na pia kuwajeruhi mitaani na vichochoroni.

Wakazi wanadai wahalifu wamekuwa wakitekeleza ujambazio wao na kisha kutoweka baadaye na kuelekea mafichoni bila ya kufikiwa na mkono wa sheria.

Kwa mujibu wa Ahmed Omar, wahalifu hao kisha hurudi mitaani baadaye na kuendelea kuwahangaisha wananchi.

Bw Omar aliitaka idara ya usalama kujukumika vilivyo na kuwatia mbaroni wahalifu hao ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

“Tumechoshwa na tabia ya baadhi ya wahalifu ambao huelekea mafichoni punde wanapogundua kuwa wanatafutwa na polisi. Wanakaa huko miezi miwili au mitatu.

Baadaye wahalifu hao hao wanarudi mitaani na kujitanua vifua huku wakiendelea kutuhangaisha. Idara ya usalama itilie maanani malalamishi haya na kuwakamata wahusika. Tumechoka kuhangaishwa vichochoroni,” akasema Bw Omar.

Wahalifu hao wanadaiwa kutumia visu, mapanga na marungu katika kutekeleza uhalifu wao.

Bi Khadija Athman alisema idadi kubwa ya vijana wanojihusisha na uhalifu huo ni wale walioacha masomo na kuingilia matumizi ya dawa za kulevya.

“Wahuni wanaotekeleza vitendo hivyo ni vijana wadodo walioacha masomo na kuingilia matumizi ya mihadarati. Lazima wakomeshwe kwani ikiwa katika umri wao mdogo wanaweza kutekeleza uhalifu huo, je wakiwa wakubwa itakuwaje? Polisi watekeleze jukumu lao ipasavyo,” akasema Bi Athman.

You can share this post!

Wakazi wa Lamu watakiwa kupanda miti maeneo wanakoishi

Baraka za ‘Nabii’ Owuor kwa wafanyabiashara...

adminleo