• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Katiba haihitaji mageuzi, Karua akosoa Uhuru

Katiba haihitaji mageuzi, Karua akosoa Uhuru

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, amekosoa vikali pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta, kwamba Kenya inahitaji mabadiliko ya kikatiba ili kukabili ghasia za kikabila ambazo hutokea kila baada ya uchaguzi mkuu nchini.

Kwenye hotuba yake mnamo Jumatatu, wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka, Rais Kenyatta alisema kuwa mabadiliko ya kikatiba ndio njia pekee ya kuondoa taharuki za kisiasa ambazo hukumba chaguzi hizo.

Hata hivyo, Bi Karua amekosoa pendekezo hilo, akishikilia kuwa ingawa hapingi marekebisho hayo, kile Wakenya wengi wanataka kuona ni utekelezaji ufaao wa katiba ya sasa.

Kwenye mahojiano mnamo Jumatatu, Bi Karua alisema kuwa ni kinaya kwamba wanasiasa wanakimbilia kushinikiza marekebisho hayo, wakati katiba ya sasa imekuwa ikikiukwa kila mara.

“Hisia zetu ni kwamba Katiba ya sasa haijatekelezwa kikamilifu, kwani kumekuwa na ulegevu mkubwa katika utekelezaji wake. Kwa hilo, sioni haja yoyote ya kushinikiza mageuzi hayo, wakati Katiba iliyopo haijakuwa ikizingatiwa,” akasema.

Baadhi ya ripoti zimekuwa zikidai kwamba Rais Kenyatta analenga kuendelea kuhudumu serikalini baada ya uchaguzi mkuu mnamo 2022, kwa kuongeza nyadhifa za kisiasa.

Miongoni mwa nyadhifa zinazotajwa ni nafasi ya Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Na ingawa amejitokeza wazi kukanusha kauli hiyo, Rais Kenyatta alinukuliwa mwaka uliopita akisema kuwa hangejali kuhudumu kwenye wadhifa wowote ikiwa Wakenya wataamua.

Hata hivyo, Bi Karua alipinga vikali kauli ya Rais Kenyatta, akishikilia kuwa tatizo kuu linaloikumba Kenya si mfumo wa utawala, bali utaratibu wa usimamizi na uendeshaji wa chaguzi kuu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

“Tatizo tulilo nalo kama Wakenya ni ukosefu wa imani kwenye chaguzi kuu na taasisi zinazoziendesha. Tunahitaji mdahalo wa kitaifa kuhusu hilo, kwani IEBC haijaimarisha uaminifu wake kwa Wakenya kwa muda mrefu, “ akasema.

Alieleza kuwa katika mfumo wowote wa kidemokrasia, lazima kuwe na mshindi na anayeshindwa, ambapo wanaokosa kuridhika na matokeo wanapaswa kwenda mahakamani kuwasilisha malalamishi yao.

Bi Karua amekuwa akikosoa juhudi zozote za mageuzi ya kikatiba, akishikilia kuwa badala yake, serikali inapaswa kuimarisha taasisi zilizopo chini ya Katiba ya sasa.

You can share this post!

Wanafunzi 2600 wakataa digrii, wajiunga na taasisi za...

Biashara zajiandaa kufungua

adminleo