Ni wikendi ya mvua, baridi na joto katika sehemu kadhaa
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imewahimiza Wakenya kujiandaa kwa mvua kubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kati ya Ijumaa, Machi 21 na Jumanne, Machi 25.
Katika ushauri wa mvua wa mwisho wa wiki uliochapishwa Ijumaa, Machi 21, Idara ya Hali ya Hewa ilionya wakazi wa Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, maeneo ya chini ya Kusini-Mashariki na Kaskazini-Mashariki mwa Kenya kujiandaa kwa mvua kubwa.
Kaunti za Nyanda za Juu Mashariki kama Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua kubwa.
Kwa mujibu wa idara ya hali ya hewa, mvua katika kaunti zilizotajwa itaanza hasa mchana na inatarajiwa kuambatana na ngurumo za radi.
Hali sawa ya hewa ilitabiriwa katika kaunti za eneo la Ziwa na Bonde la Ufa kama Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu na Elgeyo-Marakwet.
Kaunti nyingine zilizotarajiwa pia kupokea mvua kubwa ni pamoja na Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na West Pokot.
Huku mvua kubwa ikitarajiwa katika sehemu nyingi za Kenya, kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, na Taita Taveta, pamoja na maeneo ya ndani ya Tana River, zinatarajiwa kupokea mvua za wastani.
Mvua nyepesi pia inatarajiwa katika kaunti za pwani za Mombasa, Kilifi, Lamu, na Kwale, pamoja na kaunti za mashariki kama Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo.
Katika utabiri wa hali ya hewa wa siku tano, Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya pia iliwatahadharisha wakazi wa Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka, na Nairobi kujiandaa kwa baridi kali usiku.
Kwa mujibu wa utabiri, halijoto katika kaunti zilizotajwa inatarajiwa kushuka hadi nyuzi 8 kwa kipimo cha selsias kwa siku mbili za kwanza kabla ya kupanda hadi nyuzi 9 kwa kipindi kilichosalia.
Wakati huo huo, Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ilitabiri halijoto ya juu mchana katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, na Nandi.
Kaunti nyingine zilizotarajiwa kupata joto kali wakati wa mchana ni pamoja na Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo.